Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava kushoto,akiondoa kitambaa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji katika kijiji cha Tuwemacho unaotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA)kushoto kwake Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu na kulia kaimu Mkuu wa wilaya ya Tunduru Peres Magiri.
Tunduru
WAKAZI zaidi ya 3,527 wa kijiji cha Tuwemacho wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wanatarajia kuondokana na ukosefu wa huduma ya maji safi na salama,kufuatia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kuanza ujenzi wa mradi wa maji ya bomba.
Mradi huo unatekelezwa na mkandarasi kampuni ya Scorpion Ltd kwa gharama ya Sh. Sh.bilioni 1,054,232,603.55, fedha zilizotolewa na Serikali kuu kupitia programu maalum ya lipa kwa matokeo(Pfor4) na ulianza kutekelezwa mwezi Januari na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai mwaka huu.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Maua Mgallah amesema hayo jana,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava.
Alisema,mradi kwa sasa umefikia asilimia 55 ya utekelezaji wake na kazi zilizofanyika ni ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita 200,000 katika mnara wa mita tatu,ujenzi wa banio na uchimbaji wa mitaro ya kulaza bomba umbali wa mita 8,387.
Aidha alieleza kuwa,mchango wa wananchi wa kijiji hicho ni eneo walilotoa ili kupisha ujenzi wa tenk,eneo lililotumika kujenga banio na maeneo ya kupitishia mabomba ambao una thamani ya Sh.5,000,000.
Kwa mujibu wa Mgallah ni kwamba,mradi huo utakapo kamilika utaboresha kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji hicho na kuongeza kiwango cha huduma ya maji hadi kufikia asilimia 70.98 katika Halmashauri ya wilaya Tunduru.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava alisema,ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo ikiwemo ubora wake na namna Ruwasa walivyotumia taratibu za kumpata mkandarasi.
“baada ya kukagua miundombinu, nyaraka na kuangalia usimamizi ulikuwaje hivyo Mwenge wa Uhuru umejiridhisha na usimamizi wote uliofanyika kwenye mradi huo pasipo na shaka yoyote”alisema Mnzava.
Amewataka wananchi wa kijiji hicho wanaotarajia kunufaika na mradi huo kuhakikisha wana tunza miundombinu ya mradi pamoja na kutunza vyanzo vya maji.
Alisema,serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,imedhamiria kuwaondolea wananchi adha ya maji ndiyo maana inapambana kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii ikiwemo maji safi na salama.
“sisi sote tunajuwa kwamba maji ni huduma muhimu sana, na uwepo wa maji unaleta faraja kubwa kama tunavyoona akina mama wanashangilia kwa kuwa mradi huu utakuwa na manufaa makubwa” alisema Mnzava.