Kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko mkubwa wa maadili nchini Tanzania na kuathiri jamii hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa na wadau mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa njia ya maandishi kama walivyofanya wakazi wa kijiji cha Uhekule wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.
Katika uzinduzi wa Kitabu Cha Kijiji cha Uhekule Wilayani Wanging’ombe Kada wa Chama cha Mapinduzi CCM Enock Kiswaga ambaye alikuwa mgombea ubunge jimbo la Wanging’ombe mwaka 2020 amesema suala la mmomonyoko wa maadili linapaswa kuanza kudhibitiwa toka kwenye ngazi ya familia huku akipongeza jitihada za kuandika kitabu hicho ambacho amechangia kwa kununua vitabu vya zaidi ya shilingi milioni nne.
Baadhi ya waandishi wa Kitabu hicho kilichoeleza masuala mbalimbali ya Kijiji akiwemo Dokta Flown Mgani na Justin Mwinuka wamezungumzia changamoto walizokutana nazo katika ukusanyaji taarifa ikiwemo baadhi ya Wazee waliokuwa wakifuatwa kuwa na mtazamo tofauti.
Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Claudia Kitta kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo hilo Dokta Festo Dugange anasema Uhekule kimekuwa kijiji cha Mfano kwa kuandika kitabu wazo ambalo linafaa kuigwa na vijiji vingine na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao wakazi wa Kijiji cha Uhekule wamesema kitabu hicho kinawakumbusha kuenzi mila na tamaduni za kiafrika badala ya kuendekeza usasa ambao unaleta madhara hadi kwenye afya kwa kula vyakula hatarishi.
Kitabu cha Kijiji cha Uhekule kimeandikwa kwa ushirikiano na wananchi wa Uhekule wanaoishi mikoa mbalimbali ikiwa ni Kijiji Cha kwanza mkoani Njombe kuandika kitabu Cha historia yake