Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk akifungua mkutano kati ya Asasi za Kiraia na Tume Huru ya Uchaguzi kuhusu elimu ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura uliofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Juni 10, 2024.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria wa INEC Seleman Mtibora akitoa mada katika mkutano huo kati ya Asasi za Kiraia na Tume Huru ya Uchaguzi uliofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Juni 10, 2024.
…………………
KUELEKEA Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini Asasi za kiraia zimetakiwa kutumia majukwaa yao kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kuwa wapiga kura, Pamoja na kuboresha taarifa zao katika Daftari hilo ili waweze kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano mahususi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulioikutanisha Tume Huru ya Uchaguzi (INEC,) na Asasi za Kiraia zipatazo 60; Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mbarouk Salim Mbarouk amesema, Asasi za Kiraia zimekuwa zikishirikiana na Tume kwa ukaribu zaidi hususani katika wakati wa kabla na kipindi cha uchaguzi.
“Lengo la kukutana hapa ni kupeana taarifa kuhusiana na maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pamoja na masuala mengine ikiwemo uhakiki wa vituo vya kuandikisha wapiga kura, uboreshaji wa majaribio, ushirikishwaji wa wadau mbalimbali kama tufanyavyo hapa pamoja na ununuzi wa vifaa… Asasi za kiraia zina nafasi kubwa ya kufikia jamii tunaomba ujumbe na hamasa hii iwafikie wananchi kwa wakati na usahihi kupitia majukwaa yenu.” Ameeleza.
Amesema, Tume hiyo imeanza mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na rasmi uboreshaji huo utazinduliwa rasmi Julai, Mosi mwaka huu mkoani Kigoma na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa na kueleza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024/2025 umeboreshwa zaidi kwa kutumia teknolojia ya BVR (Biometric Voter’s Registration) ya kisasa zaidi kwa kuwekwa program endishi na hiyo ni pamoja na kupunguzwa uzito kwa vifaa na kubebeka kiurahisi hali itakayorahisisha kazi kwa watendaji katika maeneo mbalimbali hususani maeneo ya vijijiji.
Aidha amesema wanaendelea kukutana na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, waandishi na wahariri wa vyombo vya habari pamoja na kundi hilo la wawakilishi wa Asasi za Kiraia ili kuhakikisha elimu na taarifa zinawafikia wananchi kwa wakati na usahihi.
Akitoa Mada kuhusiana na Maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi; Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria wa INEC Seleman Mtibora amesema, idadi ya vituo 40,126 vya kujiandikisha wapiga kura vitatumika katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024/2025 huku vituo 39,709 vikiwa Tanzania Bara na vituo 417 vikiwa Zanzibar na kufafanua kuwa kuna ongezeko la vituo 2312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika 2019/2020.
“Tunataraji daftari litakuwa na wapiga kura 34,746,638 na idadi inaweza kuongezeka zaidi huku idadi ya wapiga kura 594, 494 itaondolewa kwa kupoteza sifa ya kuwa wapiga kura kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo, uraia na magonjwa ya akili yaliyothibitishwa na Daktari.” Ameongeza.
Mtibora amesema, kwa mujibu wa kanuni 15 (2) (c) za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; Tume imeweka utaratibu wa kuandikisha wanafunzi waliopo vyuoni, magereza, mahabusu na wafungwa ambao wamehukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita kujiandikisha kuwa wapiga kura.
Pia vifaa zikiwemo BVR 6000 pamoja na vishikwambi vitakavyotumika kuchukulia taarifa za wapiga kura, picha na saini vimenunuliwa huku BVR hizo zikiwa na mfumo endeshi wa Android zikiwa na kilogram 18 ukilinganisha na BVR za awali zilizokuwa na mfumo wa Windows na Kilogram 35.
Aidha amesema, Katika kutambua mchango mkubwa wa Asasi za kiraia, Asasi zenye sifa zitapewa nafasi ya kuwa waangalizi wa uchaguzi pamoja na kupewa nafasi ya kutoa elimu kwa mpiga kura na tayari maombi yamepokelewa na zoezi la uchakataji unaendelea.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wameeleza kuwa mikutano ya namna hiyo ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa ya kujadili kwa kina mambo yanayohusu Taifa na kuahidi kuibeba ajenda hiyo na kuifikisha kwa watanzania kwa msisitizo wa kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili wapate fursa ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.