NA THOMAS MURUGWA, TABORA.
Waandishi wa habari Mkoani Tabora wametakiwa kusaidia kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa Mradi wa bomba la Mafuta ghafi kutoka nchini Uganda hadi Tanzania (EACOP) katika maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini Tabora na Afisa Mawasiliano wa Nje EACOP Nchini Tanzania Bw. Abbas Abraham wakati wa semina ya siku moja yenye lengo la kuwapa taarifa sahihi waandishi wa habari ili waeze kuiambia jamii mambo gani yanafanyika katika mradi huo hivi sasa
Bw. Abraham amesema kwa kuwa wanahabari ndio kiunganishi cha mawasilino hivyo wakipata uelewa wataweza kuwaelewesha wananchi vizuri na kujua fursa wanazoweza kuzipata kwenye mradi huo.
“Tumeona tuanze kuwapa uelewa wanahabari kwenye mikoa ambayo mradi unatekelezwa ili wapate uelewa na kuweza kuwaelewesha wananchi juu ya faida za mradi huu mkubwa ambao wanatakiwa kunufaika nao,” alisema Abraham
Amebainisha kuwa ni lazima wananchi wajue kama kuna fursa mbalimbali ambazo wao wanaweza kunufaika moja kwa moja pamoja na Serikali kunufaika.
Amesema kuwa katika Mkoa wa Tabora wananchi ambao wamepitiwa na mradi wamefidiwa kwa kujengewa nyumba ambapo 14 zimejengwa Nzega, tatu katika wilaya ya Igunga na sita eneo la Sonjo ambako ndipo kuna kituo kikubwahuku wengine wakifidiwa maeneo yao ya kilimo.
Katika hatua nyingine amesema kuwa kwa kuzingatia mila na desturi za makabila mbali mbali wameweza kuhamisha makaburi 68 kwa kushirikiana na wanafamiria ambapo famiria moja wameomba wapewe muda kufanikisha zoezi hilo.
Mradi wa Bomba la Mafuta la Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Huu ni mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Kabaale – Hoima nchini Uganda kwenda kwenye peninsula ya Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania.
Mradi huu una urefu wa jumla ya kilomita 1443 kati ya hizo kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1147 zipo Tanzania na kwamba Bomba hilo vilevele linapita katika Mikoa 8 lakini pia wilaya 24, kata 134 na vijiji zaidi ya 180.
Lengo la mradi huu ni kuwezesha mafuta yatakayozalishwa nchini Uganda kusambazwa katika soko la ndani na sehemu inayobaki kuuzwa nje kwenye soko la kimataifa kupitia bomba la mafuta.