Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla Akizingumza na Viongozi na wachezaji wa Timu ya mpira ya Bara la Wawakilishi na Timu ya Arusha wazee Club katika Hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Viwanja vya Hotel ya Verde Mtoni Zanzibar.
…………………..
Na Masanja Mabula
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema ushirikiano uliopo baina ya Timu ya mpira ya Baraza la Wawakilishi na Timu ya Arusha wazee Club umekuwa ukitoa fursa mbali mbali wanapotembeleana ikiwemo kujifunza kilimo, Utalii sambamba na kuimarisha afya kupitia michezo na kuimarisha Muungano kivitendo.
Akizingumza na Viongozi na wachezaji wa Timu hizo mbili katika Hafla ya chakula cha usiku kilichoandaliwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Viwanja vya Hotel ya Verde Mtoni Zanzibar.
Amesema Serikali inathamini uhusiano unaofanyika baina ya Taasisi, Jumuia na vilabu vya Michezo kwa pande zote za Muungano kutokana na mchango mkubwa wa kimaendeleo unaopatikana kupitia Mashirikiano hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali zote mbili zitaendelea kutoa ushirikiano na kuweka mazingira bora yatakayosaidia kuimarisha umoja na mahusiano baina ya Taasisi na Vilabu vya michezo ili kuhakikisha mahusiano hayo yanadumu kwa muda mrefu na kuendelea kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni wa kihistoria Duniani.
Aidha Mhe. Hemed amewataka wenye viti wa timu hizo mbili kuendelea kuwaongoza vizuri wanachama wao na kuhakikisha wanauendeleza umoja wao ambao una mchango mkubwa katika kuimarisha na kudumisha Muungano uliotimiza miaka sitini(60) tangu kuasisiwa kwake.
Sambamba na hayo Mhe.Hemed ametoa wito kwa Timu ya Arusha wazee Club kutembelea katika maeneo mbali mbali ya vivutio vya utalii vilivyopo Zanzibar na kuwa mabalozi wazuri wa kwenda kuitangaza Zanzibar.
Mhe. Makamo wa Pili wa Rais amewataka wajumbe wa Baraza la wawakilishi na wananchi wote kuendelea kuwaunga mkono Viongozi wakuu wa nchi Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ili waweze kuwaletea maendeleo wana nchi na ifikapo uchaguzi wa mwaka 2020-2025 waendelee kuiongoza nchi.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid amepongza na kusifia uhusiano wao uliodumu kwa muda mrefu ambao umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa pande zote mbili.
Mhe. Zubeir amesema kuwa uwepo wa mashirikiano hayo unatoa fursa kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Timu ya Arusha wazee Club kufanya mazoezi ambayo yanajumuisha pande zote mbili kwa lengo la kuweka sawa Afya zao sambamba na kudumisha udugu na mshikamano ambao umeasisiwa miaka mingi iliyopita.
Mapema Mwenyekiti mwenza kutoka Timu ya Arusha wazee Club Ndugu ALLY MAMUYA amesema ushirikiano kati ya Timu hizo mbili umekuwa ni wa muda mrefu ambao umekuwa na faida nyingi ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya pamoja kwa kuimarisha Afya ya mwili na akili sambamba na kuzidi kuendelea kuutangaza utalii kati ya Zanzibar na Arusha.
MAMUYA amesema mara kwa mara wamekuwa wakipokea mialiko kutoka kwa timu ya Baraza la Wawakilishi ambayo imekuwa na tija kubwa ndani yake, hivyo ameahidi kuyaendelza mahusiano hayo kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Nae Mwenyekiti wa Timu ya Baraza la Wawakilishi Sports Club Mhe. Miraji Khamis Mussa (Kwaza) ametoa shukran kwa mabenki mbali mbali hapa nchini kwa kuwapatia ushirikiano mkubwa katika kufanikisha shuhuli mbali mbali za Baraza la Wawakilishi ikiwemo suala zima la michezo ambalo huwajenga zaidi Kiafya.
Kwaza amefahamisha kuwa michezo imewakutanisha na kuwaunganisha kati ya Wajumbe wa Baraza la wawakilishi na Timu ya Arusha wazee club mahusiano ambayo yanendelea kuzaa matunda chanya kwa pande zote mbili za Muungano.