Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrye Mnzava kushoto,akiondoa kitambaa kuashiria ufunguzi rasmi wa mradi wa maji Kamundi wilayani Nanyumbu uliotekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya Sh.milioni 800.
Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava kulia,akimtua ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Kamundi wilayani Nanyumbu Victoria Godwin baada ya kuzindua mradi wa maji safi na salama katika kijiji hicho.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Mhandisi Simon Mchucha kulia,akikabidhi taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Kamundi wilayani humo ambao umeanza kutoa huduma kwa wakazi wa vijiji viwili vya Kamundi na Mkambata.
Tenki la maji lililojengwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa vijiji vya Kamundi na Mkambata wilayani Nanyumbu.
…………
Na Mwandishi Maalum, Nanyumbu
SERIKALI imewatua ndoo kichwani wananchi wa kijiji cha Kamundi na Mkambata wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara,baada ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji ya bomba wa Kamundi unaokwenda kuhudumia wananchi 3,666 wa vijiji hivyo.
Mradi huo uliotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA),utamaliza mateso ya muda mrefu kwa wananchi wa hasa wanawake na watoto ambo awali walilazimika kusafiri umbali wa kilometa 3 kwenda na kurudi kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava,meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Simon Mchucha alisema,mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya Sh.800,000,000 kupitia programu ya lipa kwa matokeo(Pfor4).
Mchucha alisema,chanzo cha maji cha mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 7,000 kwa saa na mkakati wa kuhakikisha chanzo cha maji kinakuwa endelevu wamepanda miti 130 katika eneo la chanzo.
Mchucha alieleza kuwa,mradi huo unatekelezwa kwa mfumo wa force akaunti kupitia vikundi vya Masaka Stars kwa kazi za ujenzi na M&E Group kwa kazi za uchimbaji wa mitaro na ulazaji bomba na ulianza kutekelezwa mwezi Mei 2023 umekamilikatangu tarehe 15 Juni mwaka huu.
Kwa upande wake meneja wa RUWASA Mkoa wa Mtwara Mhandisi Primy Damas alisema,jumla ya miradi 4 yenye thamani ya Sh.bilioni 3,175,000,000 imepitiwa na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024.
Alitaja miradi hiyo ni Makome uliopo katika Halmashauri ya wilaya Mtwara,Chitoholi Halmashauri ya wilaya Tandahimba,Namatunu uliopo Halmashauri ya wilaya Masasi na mradi wa Kamundi uliopo katika Halmashauri ya wilaya Nanyumbu.
“Miradi hii imewanufaisha zaidi ya wakazi 20,000 wa vijijii hivyo,kama RUWASA iliyopewa kazi ya kusimamia huduma ya maji vijijini,kwa maana ya kubuni na kusanifu,kuijenga na kuhakikisha inakuwa endelevu tunafuraha kuona wananchi wa vijiji hivyo wanapata huduma ya maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Aidha alisema,kwa ujumla miradi hiyo imeongeza upatikanaji wa huduma ya maji vijijini katika mkoa wa Mtwara kutoka asilimia 67 hadi kufikia asilimia 74 na amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza miradi hiyo ili iwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa mujibu wa Damas,hatua hiyo itaiwezesha serikali kuongeza nguvu ya kujenga miradi mingine kwenye vijiji ambavy hakuna na huduma ya maji ili wananchi wa maeneo hayo nao waweze kunufaika na kufaidi matunda ya Serikali yao.
“Malengo ya Kitaifa ambayo pia yameainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi,inataka upatikanaji wa huduma ya maji ufikie asilimia 85 maeneo ya vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025,kwa sasa tumefanikiwa kufikia asilimia 74, lakini bado tuna miradi mingine tunajenga ikiwemo mradi wa maji Makonde”alisema Damas.
Alisema kuwa,mradi huo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi 600,000 wa mjini na vijijini,na mradi mwingine wa kutoa maji mto Ruvuma na kupeleka katika mji wa Mangaka nao utaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 100.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava,amewapongeza wataalam wa Ruwasa kwa kazi nzuri kukamilisha ujenzi wa mradi huo ulioanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Mkazi wa kijiji cha Kamundi Joseph Mpombwe,ameishukuru serikali kuwaondolea adha ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Alisema,awali walikuwa wanatembea umbali wa zaidi ya kilometa 3 kila siku kwenda kutafuta maji kwenye mito na vyanzo vingine vya asili ambavyo maji yake hayakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.