Mbunge mteule wa Jimbo la Kwahani Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharib, Zanzibar, Bw.Khamis Yussuf Mussa akinyanyua juu hati yake ya ushindi baada ya kukabidhiwa na Msimamizi wa Uchaguzi.
Aliyekuwa Mgombea wa CCM, Bw.Khamis Yussuf Mussa ‘Pele’ akifuatilia kwa makini utangazaji wa matokeo.
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupitia
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kwahani-Zanzibar Bi.Safia Iddi Muhammad imemtangaza
Bw.Khamis Yussuf Mussa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mshindi wa Kiti
cha Ubunge katika Jimbo la Kwahani.
Mussa almaarufu Pele ameibuka mshindi wa kiti hicho baada ya kupata Kura 7,092 Kati
ya Kura halali 7,383 zilizopigwa na kuwabwaga wagombea wenzake 13 waliokuwa
wakichuana katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliofanyika tarehe 8 Juni,
2024.
Jimbo la Kwahani lilikuwa na wapiga kura
11,936 na waliojitokeza kupiga kura ni 7,522 ambapo kura 139 zilikataliwa hivyo
kufanya kura halali zilizopigwa kuwa ni 7,383.
Vyama 14 vilisimamisha wagombea katika
Uchaguzi huo mdogo wa kiti cha Ubunge jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini
Mkoa wa Mjini Magharibi.
Wagombea wengine na kura walizopata katika
mabano ni pamoja na Bi. Jarade Ased Khamis wa AAFP (06), Bi. Madina Mwalim Hamad wa ADA
TADEA (49), Bi. Shara Amran Khamis wa ADC
(83), Bi. Zainab Maulid Abdallah wa CCK
(21), Bw. Abdi Khamis Ramadhan wa CUF(79), Bw.
Bashir Yatabu Said wa Demokrasia
Makaini (14) na Bi. Nuru Abdulla Shamte wa
DP(07) .
Wengine ni Bw. Kombo Ali Juma wa NRA (05), Bi. Mwanakombo Hamad Hassan wa NLD (08), Bw. Amour Haji Ali wa SAU(07), Bi. Naima Salum Hamad wa UDP(01), Bi. Mashavu Alawi Haji wa UMD(05) na Bi. Tatu Omary Mungi wa UPDP(06).
Uchaguzi katika Jimbo la Kwahani umefanyika
kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM),
Ahmed Yahya Abdulwakil (65) kufariki dunia mwezi Aprili mwaka huu.