Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
9 Juni, 2024.
KIKUNDI cha KUKAYA -Miono , Chalinze ,Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani, kimepokea mabati 72 kutoka kampuni ya Refuelling Tanzania Limited, kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya shule ya msingi Miono.
Akipokea mabati hayo kwa niaba ya kikundi cha KUKAYA MIONO ,Mwenyekiti Omary Mtiga ameishukuru kampuni ya Refuelling kwa msaada huo.
Alieleza ujenzi una miezi sita kwa nguvu zao wananchi ,wameshapokea milioni 13.5 kutoka kwa wadau, lengo lilikuwa kujenga kuongeza darasa moja lakini wamefanikiwa kujenga madarasa mawili.
Mtiga alifafanua, kwasasa bado kuna mahitaji ya mabati 34 ,malori sita ya mchanga ,maroli manne ya kokoto na mifuko ya saruji 60 ili kukamilisha ujenzi huo.
“Tunashukuru uongozi wa kampuni hii, chini ya Mkurugenzi Mohsin Bharwani ambae ameguswa na jambo hili, Mohsin amekuwa akijitoa katika masuala ya kijamii kwenye maeneo mengi ndio na sisi tuliamua kumuomba msaada na tunashukuru kutusaidia “
Aidha Mtiga alitoa wito kwa makampuni na wadau wengine kuendelea kujitolea kwani bado kuna uhitaji.
Aliiomba jamii Miono kuendelea kushirikiana katika masuala ya maendeleo ili kujiinua kimaendeleo ikiwemo kuboresha sekta ya elimu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni ya Refuelling Tanzania limited, Mohsin Bharwani, Meneja wa kampuni hiyo Renatus Kabeyo alisema wamekabidhi mabati 72 na kusafirisha jumla milioni mbili (mil.2).
Alifafanua kuwa, kampuni hiyo inashirikiana na jamii kwa kila jambo kulingana na uwezo wao.
“Nimeona kuna madarasa tunaona mnajenga ,vyoo ,niweze kuahidi tutajenga hoja ,pamoja na misaada inayokuja nikuombe ofisa elimu kata andika andiko ,ili mpate misaada mikubwa kutoka kwa wadau mbalimbali” alieleza Kabeyo.
Kabeyo alisema wanafunzi wanasoma ila wanatakiwa kusoma kwenye mazingira bora.