Na Mwandishi Wetu WHMTH, Arusha
TANZANIA imependekeza iwe na mwakilishi kiongozi katika nafasi ya juu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU).
Pendekezo hilo limetolewa Juni 5, 2024 na wawakilishi wa Tanzania katika Kamati ya Fedha na Utawala kwenye vikao vya wataalamu wa masuala ya Posta vinavyoshirikisha wajumbe kutoka mataifa 46 wanachama wa PAPU.
Wamesema msingi wa pendekezo hilo unazingatia mkataba wa nchi mwenyeji kutakiwa kuchangia asilimia 50 ya bajeti ya uendeshaji ya PAPU kila mwanzo wa mwaka wa fedha iwapo nchi wanachama hazijachangia kwa wakati; fedha ambazo baadaye hurejeshwa.
Aidha, wawakilishi hao katika hoja zao wamesisitiza kuipata nafasi hiyo ili kuhakikisha usimamizi imara wa fedha zinazotolewa ambazo Tanzania imekuwa ikilipa kama nchi mwenyeji ili kupata marejesho ya gharama za ujenzi ilizolipa zaidi ya kiwango chao cha umiliki cha asilimia 40.
Kwa upande wa Kamati ya Mkakati (Strategy), wajumbe walionesha mchango mkubwa wa Tanzania katika ujenzi wa jengo la PAPU lililo Jijini Arusha ambapo mwaka huu Mkutano wa 42 wa Baraza la Umoja wa Posta Afrika unafanyika.
Kamati hii imefikia maazimio ya kuunda kikosi kazi katika kamati ya mkakati kitakachoshughulikia upanuzi na ushirikishaji watoa huduma katika Sekta ya Posta ambapo Tanzania imejitolea kushiriki pamoja na nchi za Botswana, Burkina Faso, Cameroon, DRC, Ivory Coast, Kenya, Misri, Namibia, Niger na Uganda.
Wajumbe hao pia wamejadili masuala ya mapato na matumizi ya umoja, miradi, ajira na stahiki za watumishi wazawa, michango ya ada za uanachama na mpango mkakati wa miaka minne wa Sekta ya Posta barani Afrika ili iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.