Wapiga kura 11,936 wanatarajiwa kupiga kura kesho tarehe 09 Juni, 2024 kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kwahani lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele ameyasema hayo leo tarehe 07 Juni, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akisoma risala kwa ajili ya uchaguzi huo na kuongeza kwamba uchaguzi utahusisha vituo 29 vya kupigia kura.
“Jumla ya wapiga kura 11,936 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) watashiriki katika uchaguzi huu mdogo na jumla ya vituo 29 vya kupigia kura vitatumika,” amesema Jaji Mwambegele.
Wagombea wanaowania Kiti cha Ubunge jimbo la Kwahani majina yao na vyama katika Mabano ni Bw. Bashir Yatabu Said (Demokrasia Makaini), Bi. Nuru Abdulla Shamte (DP), Bi. Mwanakombo Hamad Hassan (NLD), Bi. Zainab Maulid Abdallah (CCK), Bi. Tatu Omary Mungi (UPDP), Bw. Khamis Yussuuf Mussa (CCM) na Bi. Jarade Ased Khamis (AAFP).
Wengine ni Bw. Kombo Ali Juma (NRA), Bi. Shara Amran Khamis (ADC), Bi. Naima Salum Hamad (UDP), Bi. Madina Mwalim Hamad (ADA TADEA), Bw. Amour Haji Ali (SAU), Bi. Mashavu Alawi Haji (UMD) na Bw. Abdi Khamis Ramadhan (CUF).
Mwenyekiti wa Tume amevikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala wa vyama, wapiga kura na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kwamba hawapigi kampeni siku ya kupiga kura kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
“Alama za vyama vya siasa zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi haviruhusiwi kutumika kesho tarehe 08 Juni, 2024 ambayo ni siku ya uchaguzi,” amesema.
Jaji Mwambegele ameongeza kwamba zoezi la kupiga kura katika maeneo yote ya uchaguzi litafanyika katika vituo vilevile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
Ameongeza kwamba vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni.
“Iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi kamili (10:00) jioni katika mstari na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa kumi kamili (10:00) jioni,” amesema.
Jaji Mwambengele amebainisha kwamba watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Amesema, Tume imeandaa majalada ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kuona kupiga kura bila usaidizi. Aidha, Kwa wapiga Kura wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo, wataruhusiwa kwenda vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.
“Katika kituo cha kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokwenda na watoto kituoni,” amesema.
Kuhusu wapiga kura kurudi nyumbani baada ya kupiga kura, Jaji Mwambegele amesema hilo ni sharti la kisheria na kwamba maadili ya uchaguzi yaliyosainiwa na kuridhiwa na vyama vyote vya siasa, Serikali na Tume yanaelekeza hivyo.
Alisisitiza kwa kusema “wapiga kura watatakiwa kuondoka kituoni mara wanapomaliza kupiga kura ili kuepusha msongamano na vitendo vinavyoweza kuchochea uvunjifu wa amani. Hivyo, Tume inawashauri wananchi kujiepusha na mikusanyiko katika maeneo ya vituo vya kupigia kura”.
Ametoa rai kwa wapiga kura katika Jimbo la Kwahani, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura, ili kuwachagua viongozi wanaowataka.