Mkuu wa Dawati la Sheria Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke Wakili Mwanakombo Rajab akizungumza na mwandishi wetu leo Juni 7, 2024 jijini Dar es Salaam.
………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imemfikisha Mahakamani Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam Victoria Mwasonya (64) kwa tuhuma ya kughushi nyaraka za fomu ya ardhi namba 73 kwa lengo la kujipatia hati ya umiliki wa ardhi jambo ambalo ni kinyume cha kifungu kidogo cha kwanza D 333, 335 na 337, 342 kwa mujibu wa sheria za mwendesha wa Mashitaka ya Jinai.
Akisomewa hati ya Mashitaka leo Juni 7, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Temeke Mhe. Ally Mkama, Mtuhumiwa Victoria Mwasonya (64) amedaiwa amefanya makosa mawili ikiwemo kughushi nyaraka pamoja na kuwasilisha taarifa za uongo Manispaa ya Temeke kitengo cha ardhi ili kujipatia hati miliki.
Mtuhumiwa amekana makosa yake na kurudishwa mahabusu baada ya kukosa mdhamini, huku kesi hiyo ikitarajiwa kusikilizwa tena Juni 26, 2024.
Akizungumzia kesi hiyo, Mkuu wa Dawati la Sheria TAKUKURU Mkoa wa Temeke Wakili Mwanakombo Rajab, amesema kuwa mwaka 2021 walipokea taarifa kuhusu Mkazi wa Kata ya Sandali, Mtaa wa Mambo leo A, Manispaa ya Temeke Victoria Mwasonya amechukua mkopo benki wa shilingi milioni 25 na kuweka dhamana nyumba ya jirani yake bila mmiliki kuwa na taarifa.
Wakili Rajab amesema kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo walianza kufanya uchunguzi pamoja na kumtafuta mtuhumiwa ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo.
Amesema kuwa inadaiwa mtuhumiwa katika nyaraka hizo alighushi saini ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mambo leo A pamoja na Afisa Mtendaji Kata ya Sandali na nyaraka kuonesha wamelinzia kuwa yeye ni miliki wa eneo na nyumba.
Imeelezwa kuwa Manispaa ya Temeke kitengo cha ardhi walipokea nyaraka hizo kutoka kwa mtuhumiwa huyo na kuzifanyia kazi, kisha kumpatia leseni ya makazi yenye namba TMK 0354 ambayo inaonesha yeye ni mmiliki halali wa nyumba pamoja na eneo hilo lililopo Kata ya Sandali.
“Baada ya kupata leseni ya makazi alienda kuomba mkopo benki wa shilingi milioni 25 kwa makubaliano ya kulipa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, mtuhumiwa aliondoka katika mtaa huo na muda ulipofika wa kulipa deni benki walitaka kuuza nyumba, ndipo wamiliki wakaja kutoa taarifa TAKUKURU Mkoa wa Temeke” amesema Wakili Rajab.
Amesema kuwa waliendelea na uchunguzi pamoja na kumtafuta mtuhumiwa katika maeneo yote na Juni 4, 2024 walifanikiwa kumkamata akiwa Mkoa wa Mbeya.
“TAKUKURU Mkoa wa Mbeya walifanikiwa kumkamata na kutupa taarifa, hivyo baadhi ya Maafisa kutoka TAKUKURU Mkoa wa Temeke walikwenda kumfata na kumleta Mkoa wa Dar es Salaam ili kujibu tuhuma zinazomkabli na leo asubuhi tumemfikisha katika Mahakamani ya Wilaya ya Temeke” amesema Wakili Rajab.