TUME ya TEHAMA nchini (ICTC) imeingia makubaliano na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogovidogo Tanzania (SIDO) ili kufanikisha vituo vya ubunifu ambavyo vitawasaidia vijana kuweza kukuza kampuni zao za ubunifu nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Juni 6,2024 katika ofisi za SIDO makao makuu jijini Dar es Salaam ambapo kwa kuanzia, mameneja wa mikoa sita wa SIDO wamesaini mikataba na tume kwa ajili ya utekelezaji huo.
Aidha, mameneja waliosaini mkataba na tume ni kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mbeya, Mwanza na Lindi.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Mkundwe Moses Mwasaga amesema, makubaliano hayo ya kihistoria yamelenga kuwezesha vijana wa Kitanzania kuneemeka kupitia Uchumi wa Kidijitali.
“Leo hii sisi tunafurahi sana, kwa hii shughuli tuliyofanya ya kusaini hayo makubaliano sita ya mikoa sita katika programu kubwa, ambayo tunapanga hiyo programu ifike Tanzania nzima.”
Dkt.Mwasaga amesema,programu hii imelenga vijana na wanachofanya, wamekubaliana na wenzao SIDO.
“Kwa sababu SIDO ndiyo incubator na acceleretor ya kwanza Tanzania.Na ndio kubwa na ndio yenye maeneo mikoani kote, sisi tunachofanya nao ni kwamba tunajenga vituo vya ubunifu.”
Amesema, vituo hivyo vya ubunifu vitawasaidia vijana kuweza kukuza kampuni zao za ubunifu nchini.
“Tume, katika moja ya kazi yake katika kukuza TEHAMA Tanzania ni kuhakikisha kwamba, Tanzania inakuwa na uchumi wa kidigitali ambao huo uchumi unakuwa unajengwa na kampuni ndogo ndogo nyingi za vijana.
“Kwa hiyo mahusiano yetu na wao ni mahusiano ambayo yote tunaongezeana nguvu katika kuhakikisha kulifanikisha hilo.”
Aidha, kuhusu vijana wangapi ambao watahusika na jambo hilo, Dkt.Mkundwe amesema, “TEHAMA kama mnavyoifahamu ina watu wa aina mbili ukiondoa watumiaji.
“Kuna kampuni ambazo zinatumia TEHAMA ili kufanya shughuli anayoifanya iende vizuri zaidi.
“Ni kama hao ambao mnaona wanatumia Instagram na vitu vingine, halafu kuna kampuni zingine zenyewe biashara yake ndiyo TEHAMA.
“Sasa hao wote ni wanufaika wa hivi vituo tunavyovijenga. Na tumeanza na vituo sita na ukiondoa hivyo sita, viwili ambavyo vitakuwa katika mikoa hiyo hiyo ni vituo vya kutengeneza bidhaa za TEHAMA.
“Kwa hiyo, hapa tunaangalia tu kwamba siyo suala la kutengeneza kampuni ambalo tutatengeneza mifumo tu, lakini tutazisaidia kampuni ambazo zitakuwa zinatengeneza vifaa vya TEHAMA.
“Na hilo linaendana na adhima ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba tunaujenga uchumi wa kidigitali wa Tanzania ambao unakuwa define na kampuni za vijana.
“Kwa sababu wote tunafahamu kwa Tanzania sasa hivi, vijana tulio nao ni takribani milioni 21 kutokana na Sensa tuliyofanya iliyopita.”Amesema, hao vijana wanatakiwa wawajengee uwezo wa kibunifu ili waweze kutengeneza makampuni.
Dkt.Mwasaga amesema,wakitengeza hayo makampuni yatakuwa yanafanya vitu viwili vikubwa ambavyo tume imeundwa kwa ajili yake.
“Cha kwanza kutengeneza ajira kwa vijana na cha pili kufanya Sekta ya TEHAMA iweze kutoa mchango mkubwa kwenye Pato Kuu la Taifa la Tanzania.Kwa hiyo hayo ndiyo mambo ambayo tunayaangalia.”
Amesema, gharama za vituo hivyo sita ambayo inahusiana na ukarabati wa maeneo na pia kuweka vifaa vinavyotakiwa ni zaidi ya shilingi bilioni 8 za Kitanzania ambazo zitahusika katika mambo hayo.
“Na huu mradi utaenda nchi nzima ili tuweze kuhakikisha kwamba, vijana wanakuwa na chachu ya kuanzisha makampuni, kwa sababu wote sasa hivi tunafahamu kuna soko huru la Afrika ambapo Tanzania sasa hivi ni mwanachama.
“Tunataka hawa vijana wetu, bunifu zao zieweze kupata masoko Afrika nzima ikiwezekana na vile vile waweze kushindana duniani.
“Kwa hali ya sasa hivi, nadhani wote mnafahamu mifumo mingi tunayoitumia hasa kwenye masuala mfano ya mitandao ya kijamii na vitu vingine haikutengenezwa Tanzania.
“Kwa kutumia hivi vituo, tutawapa ujuzi vijana, tuweze kutengeneza mifumo yetu ya Kitanzania, tuweze kupata soko la hapa na soko la nje.
“Na wote, sisi tunafahamu kabisa Tanzania sisi kwenye ushindani tuna bahati, Kiswahili kimewekwa katika lugha za Afrika, kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kutengeneza mifumo mbalimbali ambayo itakifanya Kiswahili kiweze kutumika sehemu mbalimbali.
Hiyo hizo ndiyo sehemu ambazo tutakuwa tunafanya hivyo, tunaprogramu mbalimbali tunaweza kuwakutanisha watu wa mabenki, watu wa kisheria, watu wa kutengeneza kampuni na vitu vingine ili kuwasaidia hawa vijana waweze kuanzisha kampuni nyingi ili tuweze kujenga uchumi wa kidigitali ambao ni shindani kwa Tanzania.”


