ZIARA za Rais Samia Suluhu Hassan zinalipa. Hivyo ndivyo unaweza kusema kutokana na maelezo ya mawaziri walioambatana na kiongozi huyo kufunguka mazito.
Mawaziri hao wamefunguka mazito hayo leo wakati wakizungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni muda mchache baada ya kuwasili kutoka nchini Korea ambapo Rais Samia alifanya ziara ya kiserikali na kushiriki mikutano mbalimbali.
Baadhi ya Mawaziri waliozungumzia ziara hiyo ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Fedha Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu El Maamry.
Akizungumzia ziara hiyo Waziri Mkumbo amesema kupitia ziara hiyo Tanzania inaenda kunufaika kwenye sekta ya madini mkakati ambapo Rais Samia amezungumza na wawekezaji wakubwa wa Korea kuja kuwekeza mitambo ya kuchakata raslimali hizo hapa nchini ili kuongeza thamani.
“Tunataka wawekezaji ambao watakuja Tanzania na kuwekeza katika sekta ya madini kwa kuhakikisha madini yanachakatwa hapa hapa ili tuamini iweze kuongezeka na nchi iweze kunufaika. Jambo la kushukuru ni kwamba wawekezaji wameonesha kukubali,” amesema Mkumbo
Waziri huyo amesema mkakati wa kuongeza thamani rasiliamali unahusu sekta zote hivyo kuwataka watanzania waongeze kasi ya kufanya kazi.
Amesema katika kunufaika na Korea, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesaini mkataba na kampuni kutoka Korea ambayo itakuwa inatoa taarifa na kuandaa program za wawekezaji kutoka nchi humo.
Waziri Mkumbo amesema serikali imeweka mkazo katika nchi za Asia na Afrika ambazo zimeonesha kuhitaji ushirikiano wa kiuchumi.
Amesema mkopo wa dola za Marekani bilioni 2.5 ambao unatarajiwa kulipwa baada ya miaka 26 kwa riba ya 0.01 ndani ya miaka 40 unaenda kuleta mapinduzi kwenye sekta mbalimbali nchini.
Aidha amesisitiza kiwa taarifa za kuwa mkopo huo una masharti ya kutoa sehemu ya bahari hazina ukweli na haiwezi kutokea katika ulimwengu wa sasa. Kwa upande wake Waziri Nape amesema ziara hiyo inaenda kunufaisha serikali katika sekta ya TEHAMA ambayo ni muhimu kwa uchumi wa sasa.
Amesema pia wameweza kuzungumza namna ya kushirikiana katika eneo la STARTUP ambalo limekuwa na mchango mkubwa wa kuzalisha wawekezaji mbalimbali. Amesema Wizara yao inatarajia kujenga Chuo cha TEHAMA mkoani Dodoma ambapo kwa sasa wamekamilisha upembuzi yakinifu.
“Tumetembelea kituo kikubwa cha kusaidia bunifu zinazobuniwa na vijana wa Korea na wanazitumia kwenye kuibua fursa mbalimbali zinazosaidia uchumi wao,” amesema.
Waziri Nape amesema ziara hiyo imewaonesha ni namna gani tunapaswa kubadilika katika kufanya kazi ili tuweze kuendelea kwa haraka. Naye Waziri wa Mkuya amesema ziara hiyo imewezesha ndoto ya muda mrefu ya Zanzibar ya kujenga Hospitali ya Mbinguni ambayo itaweza kutoa huduma za kibingwa kama matibu ya moyo, wakina mama na watoto.
“Tumepata takribani Sh bilioni 400 za ujenzi wa Hospitali ya Mbinguni Zanzibar, hili limefanyika kutokana na juhudi za Rais Samia,” amesema.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Kijaji amesema ziara hiyo imewapa funzo la namna ya kuuza bidhaa za Tanzania kwenye soko la dunia. Dk Kijaji amesema Wizara yake itahakikisha fursa zote ambazo zinapatikana kwenye soko la dunia wanazitumia ili kuhakikisha mnyororo wa thamani unaongezeka kwa haraka.
Katibu Mkuu Dk El Maamry amesema Tanzania inaenda kufanya mapinduzi katika sekta ambazo zitanufaika na mkopo huo wenye masharti nafuu. ” Tunaenda kukaa na kuchakata ni eneo gani tunaona linafaa kunufaika na mkopo huu, halafu tunawaambia wenzetu wa Korea ili tuweze kwenda kwenye utekelezaji,” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema hakuna mjadala kuhusu muelekeo wa Serikali ya Rais Samia kwamba safari zake za nje, zina uhusiano mkubwa na maendeleo ya nchi.
Aidha, amesema Watanzania ni mashahidi kuwa kuna wakati Tanzania ilijaribu kufunga milango ya ushirikiano na nchi za nje, na matokeo yake kwenye sekta ya uwekezaji, biashara na hata sifa na heshima ya Tanzania ikashuka.
Amesema kwa mujibu wa sera mambo ya nje ya mwaka 2001, inaitaka Tanzania kuchangamana kimataifa ili kutimiza malengo ya kimaendeleo.
Amesema katika misingi saba ya sera hiyo, msingi namba tano ni ushirikiano kimataifa wa maendeleo.
“Dunia ya sasa ni ya ushindani lakini pia ni ya ushirikiano, nchi zinashindana kupata masoko na maarifa katika maendeleo. Pia kuna changamoto za kidunia zinahitaji ushirikiano mfano mabadiliko ya tabia nchi.
“Kwa maana hiyo maarifa ya viongozi lazima yaguse ushirikiano na ushindani na katika kupata yote lazima kutafuta washirika ili kuhimili ushindani na kujenga uwezo na kutimiza malengo ya maendeleo.
“Hivyo kwa dunia ya sasa hamna namna ya kukaa ndani ya mipaka yako bila kutoka bila kuzungumza na dunia ukaamini utatimiza malengo yako, haitapata kutokea,” amesema.
Amesema Watanzania hujisifu tangu zamani kwamba nchi inaheshimika duniani kuliko uwezo wa kiuchumi na kijeshi lakini sifa hiyo haijaja kwa ajali bali imejengwa kwa viongozi wake tangu awamu ya kwanza kushirikiana na dunia.