Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Dodoma.

Raslimali watu ni nyenzo muhimu katika kufanikisha mipango, mikakati na maendeleo ya taasisi na nchi. Ili mipango na malengo iliyowekwa iweze kutimia na kutekelezwa ipasavyo ni lazima raslimali watu waingie kazini kuifanikisha kwani bila kufanya hivyo mambo yatakwama kabisa. 
Ikumbukwe kuwa ili wafanyakazi ambao ni raslimali waweze kutimiza majukumu yao kikamilifu, ni lazima pawepo na uratibu na usimamizi thabiti wa majukumu yao ya kila siku.

Maofisa utumishi wanawajibika kuwasimamia watumishi na kuhakikisha wanapata haki zao stahiki kwa mujibu wa kanuni, sheria na miongozo iliyopo.
Maofisa utumishi wana majukumu kadhaa, miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na kupima utendajikazi wa watumishi, kushughulika masuala ya nidhamu na malalamiko ya watumishi, kuratibu vikao, likizo na mafunzo kazini, kushughulikia mikopo na malimbikizo ya watumishi pamoja na kupandisha vyeo na madaraja kwa watumishi baada ya kupata kibali kutoka ofisi kuu ya utumishi au mwajiri. 

Endapo maofisa utumishi hawatatimiza majukumu yao ipasavyo, watumshi watakuwa na malalamiko, huzuni na hata kuchukia utumishi wa umma kwani watakosa haki zao muhimu zenye uhusiano wa moja kwa moja na ustawi wao kiutumishi na kimaisha pia.
Suala la maofisa utumishi kushughulikia masuala ya watumishi si ombi wala hisani bali ni jukumu lao la msingi ambalo ni miongoni wa majukumu yao katika mikataba ya ajira zao na hulipwa mishahara na posho mbalimbali kwa kazi hizo. 
Ni muhimu kwa maofisa utumishi kukumbuka mara zote kuwa wao ni kiungo muhimu katika kufanikisha utendajikazi wenye ufanisi unaopelekea tija mahali pa kazi na maendeleo ya taifa.

Ni katika muktadha huo, wanapaswa kutimiza majukumu yao kikamilifu ili watumishi wajikite kuchapa kazi badala ya kutumia muda mwingi kusafiri mara kwa mara kufuatilia stahiki na madai yao maofisini kwa masuala ambayo yangeweza kutatuliwa endapo maofisa utumishi wangetimiza wajibu wao ipasavyo.

Mei 4, 2024, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete alifungua mkutano wa 11 wa wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Utumishi wa Umma na Uongozi (AAPAM), Tawi la Tanzania jijini Arusha. 
Katika mkutano huo, Ridhiwani Kikwete aliwasihi maofisa utumishi kuwatendea haki watumishi na kuacha uonevu na roho mbaya dhidi yao. “Acheni kuwa na roho mbaya, hayo matendo yenu mabaya hayawapendezi hata kidogo, kuweni na huruma, hiyo nafasi uliyonayo haidumu, usijione mungu mtu, nataka muwe kimbilio la wenzenu,” alisema Ridhiwani Kikwete.
Kimsingi, Ridhiwani anakumbusha kuwa cheo ni dhamana na daima haipaswi kutumia nafasi yako kuwaumiza wengine badala yake ninkuwasaidia kupata haki zao na hatimaye kuongeza tija kazini. Pia, anataka watumishi wanapokuwa na shida yeyote basi wajisikie huru kuwaambia maofisa utumishi wao wakijua masuala yao yatapatiwa ufumbuzi badala ya mtumishi kutafuta haki yake kwa kusafiri umbali mrefu kwenda wizarani jijini Dodoma. 

Katika mkutano huo, Naibu Waziri huyo alikemea vikali tabia ya baadhi ya maofisa utumishi wasio waaminifu wanaofikia hatua ya kuwawekea kauzibe watumishi wanaowasimamia ili wasipate fursa za mafunzo, safari za kikazi, semina, warsha na kupandishwa vyeo kutokana tu na roho mbaya na husuda.
Binafsi nashindwa kuelewa ni faida gani anayopata ofisa utumishi anapoweka kauzibe dhidi ya mtumishi mwenzie ili tu asipande daraja au kukosa stahiki zake. Kwangu mimi naona hii ni zaidi ya roho mbaya na uonevu uliopitiliza. Halafu najiuliza pia, fedha anazolipwa mtumishi kutokana na kusafiri kikazi, kupanda daraja au cheo ni fedha za serikali wala hazitoki mfukoni mwa ofisa utumishi, yeye ofisa utumishi anaumia nini hadi kufikia hatua kumwekea kauzibe mtumishi mwenzie? Inashangaza na kustajabisha kwa kweli ndugu msomaji.

Ndiyo maana moja ya tafsiri ya neno husuda ni kutopenda maendeleo ya mwingine hata kama hayakuathiri chochote wewe au kutamani neema alizopewa mwenzako zimtoke hata kama unajua wewe haziji kwako!
Ni kile kitu ambacho mwanasiasa Mudhihiri Mudhihiri aliwahi kuita tabia za nyoka wa mdimu. Kwamba nyoka huyu hali matunda husika (ndimu) lakini ukipanda kwenye mti huo ili kuangua ndimu na yeye kajificha kwenye mti huo anakugonga! Kama hiyo haitoshi, katika kukazia umuhimu wa maofisa utumishi kuwatendea haki watumishi na wafanyakazi wanaowasimamia kazini, Mei 20, 2024, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akiwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wataalamu wa Raslimali Watu na Utawala ambapo kitaifa yalifanyika mkoani Morogoro aliwataka maofisa utumishi kuwatendea haki wafanyakazi wote kwa kujiepusha na vitendo vyovyote vya uonevu. 
“Ni muhimu sana tukumbushane kuwa tuna dhima kubwa ya kusaidia kujenga na kuimarisha nguvu kazi endelevu katika maeneo yetu ya kazi na kwenye ofisi zetu. Taaluma yetu hii itaendelea kuhitajika na kuheshimiwa sana iwapo sote tutatimiza wajibu wetu wa kuhakikisha watu wanapata haki na maslahi yao. Baadhi yetu waache kujifanya miungu watu, wanaonea watu na kutisha watu. Unakalia faili la mtu mwaka mzima. Tuache hizo tabia mbaya,” alisisitiza Dk. Nchimbi.

Alichokiongea Balozi Dk. Nchimbi ni muhimu sana kuzingatiwa kwani miongoni mwa vitu vinavyoongeza hamasa, ari na mwamko wa kufanya kazi kwa bidii, ni pale haki, maslahi na stahili mbalimbali za wafanyakazi zinapotekelezwa ipasavyo kupitia utendajikazi mahiri wa maofisa utumishi.

Hakuna haja ya ofisa utumishi kuonea, kutisha na kuminya haki ya mfanyakazi kwani ni kosa kisheria lakini pia linakiuka maadili na miiko ya utumishi wa umma. Si jambo la afya kwa ofisa utumishi kujiona mungu mtu kwa kuchelewesha kupatikana kwa haki ya mfanyakazi ambaye yeye anawajibika kuhakikisha anapata haki yake kwa wakati. 

Matumizi ya lugha nzuri dhidi ya wafanyakazi katika kuwajibu na kuwaelekeza jambo ni muhimu yazingatiwe na maofisa utumishi ili kuendelea kuwapa watumishi vicheko katika utumishi wao.

Pia, Dk. Nchimbi alisisitiza haki za msingi za wafanyakazi akisema ni lazima zizingatiwe kikamilifu. “Watu wapande madaraja yao kwa merits (sifa) zao, wapate vyeo kwa merits, wapate safari kwa merits. Watu wapate madai yao, mishahara, posho, likizo… hizo zote ni haki za watu. Tusimamie haki za watu bila haya. Msionee mtu wala kuleta undugu au kuomba rushwa ndiyo mtu apate haki na maslahi yake. Kila mmoja wetu atambue analo deni la kutumikia watu kwa kutanguliza maslahi ya taasisi na watu mbele, kuliko maslahi yake binafsi,” amesema Balozi Dk. Nchimbi.

Upo uhusiano wa moja kwa moja wa uzembe au roho mbaya ya ofisa utumishi katika kusababisha wafanyakazi kukosa haki na maslahi yao muhimu. Mathalani, endapo ofisa utumishi atashindwa kutuma taarifa za watumishi ambazo kupitia taarifa hizo wafanyakazi watapata haki zao, basi ni dhahiri, wafanyakazi watakosa haki zao kama vile kulipwa fedha za likizo, kupanda madaraja na vyeo na hata kukosa kulipwa mafao kwa wakati kwa wale wastaafu.
Kuna haja ya maofisa utumishi kubadilika sasa na kuwatendea haki watumishi na wafanyakazi wanaowasimamia. 

Iko taasisi moja ya umma yenye watumishi zaidi ya 300, mmoja wa maofisa utumishi alihamishiwa taasisi nyingine lakini baada ya muda watumishi waliandamana kwa Mkurugenzi Mkuu kuomba arudishwe ‘mtu wao’ kwani maofisa wengine waliobaki kwenye idara/ofisi hiyo watumishi walikuwa hawawaelewi kwa maana ya kutojali kwao, lugha zao na utendaji usioridhisha kwa ujumla. Hivi kwenye ofisi kama hiyo na ikawa miongoni mwa maofisa waliobaki na ambao wafanyakazi wanawalalamikia unajisikiaje?

Kipo pia kisa cha taasisi nyingine ya umma ambayo ofisa utumishi wake mmoja alipostaafu ilikuwa mithili ya msiba. Wafanyakazi takribani wote walieleza namna walivyokuwa wanajisikia vibaya kujitenga naye. Alikuwa ni mtumishi kweli wa watumishi ambaye halali mpaka aone kero ya mtumishi inatatuliwa.
Kwa nini ofisa utumishi (hata kiongozi mwingine) usiwe miongoni mwa maofisa utumishi ambao uwepo ni kama nuru muhimu inayowaangizia njia watumishi wote na kukosekana kwao ni sawa na nuru hiyo kuzimika?

Kiongozi na mfanyabishara mkubwa wa zamani wa Morocco, Abu Abd Allah Muḥammad ibn AbdAllah Al-Lawati aliyejulikana zaidi kwa jina Ibn Battuta alipata kusema: “Tunafanya haya katika kusaidia matatizo ya watu wetu ili hata tutakapokufa, watu wasitutafute kwenye makaburi yaliyonakshiwa kwa marumaru na chokaa bali katika mioyo ya wale walionufaika kwenye maisha yao kutokana na sisi.”
Kwa nini na wewe ofisa utumishi au kiongozi mwingine yeyote usiwe ambaye utaingia kwenye mioyo ya watu kwa jinsi unavyojitoa katika kusimamia maslahi yao? Katika Biblia, Neno la Mungu katika Kitabu cha Mithali 14:34, linasema “Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wowote.” Pia, Mithali 3:27 inasema “Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.”

Lakini kwa wenzetu Waislamu, hadithi ya Mtume Muhammad (SAW) inasema kwamba “Mtu anayependeza sana mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule ambaye watu wengi wananufaika naye.” Maofisa Utumishi na wengine wote wenye mamlaka wanayo nafasi ya kuinua taifa letu kwa kutoa haki bila kumwonea mwingine. Haki ikitamalaki, furaha na vicheko huwa ni sehemu ya maisha ya kila siku.

Mungu Ibariki Tanzania.

Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.