Na Joel Maduka,Geita..
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa imetoa mafunzo kwa Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita kuhusu kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta na kanuni za maudhui ya mtandaoni ya mwaka 2020.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita , Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Imelda Salum ,amewataka Waandishi wa habari na vyombo vya habari kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazotakiwa ili kuepuka migongano isiyokuwa ya lazima.
“Ni vyema waandishi hususani wa mitandaoni wakazingatia maadili na misingi ya weledi wa taaluma yao itatusaidia sisi kutambua misingi imara ya shughuli ambazo wanazifanya hatupendi kuwa kikwazo kwa waandishi kutekeleza majukumu yao lakini wanapofikia hatua ya kutulazimisha ndio maana na sisi tunafuata misingi ya sheria ambayo tumeiweka”Imelda Salum Meneja TCRA
Aidha ameongeza kuwa waandishi wa Habari na wanahabari ni wadau muhimu kwenye sekta ya Habari na kwamba wanatambua ni muhimu kwa kundi hilo kutambua kanuni na sheria ambazo zimewekwa kwa lengo la kuepukana na makosa ambayo yanaweza kuwapelekea kupigwa faini au kufungiwa chombo husika ambacho kinakuwa kimekiuka kanunia na sheria za mawasiliano.
“Kama tunavyofahamu kwa sasa hivi ulimwengu wa Teknolojia vyombo vingi kama Televisheni ,Radio na Magazeti wamekuwa ni wadau wa Habari za mitandaoni kwa hiyo ni muhimu kwa wausika wa vyombo hivi kuwa na uelewa mzuri wa kazi ambazo wanazifanya ziwe na misingi bora ya kuwafikia wananchi” Imelda Salum Meneja TCRA
Mhandisi Salum ameongezea kwa kuwashauri wananchi wanaofanya malipo yoyote ya serikali wahakikishe wanafanya kwa Control number ili kuepuka utapeli na ujanja ujanja unaofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu.
Katika hatua nyingine Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa wito kwa wanataaluma ya habari kuchukua tahadhari na kuwa makini wakati wanapotoa taarifa zinazohusu masuala ya Uchaguzi.