……..
Zaidi ya wadau wa mifugo 300 wanatarajiwa kushiriki Maonesho ya Mifugo na mnada yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 14- 15, 2024 katika viwanja vya Ubena Estate Chalinze Mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 5, 2024 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kibiashara wa Ng’ombe(TCCS) Naweed Mulla, amesema kuwa lengo la kuanzisha maonesho hayo kusaidia wakulima na wafugaji kujikwamua kiuchumi pamoja na kuongeza pato la Taifa kupitia ufugaji.
Mulla amesema kuwa washiriki 300 wanatarajia kuhudhuria maonesho hayo ambayo yatafanyika kwa siku tatu yakiwa na lengo la kuwawezesha wafugaji, wasindikaji na wadau mbalimbali nchini ili kushawishi sera za maendeleo na kukuza uzalishaji wa mifugo endelevu kwa njia ya kuwajengea uwezo na mitandao.
Amesema kuwa maonesho hayo yana nia ya kuwezesha Jukwaa Madhubuti la Kitaifa la wafugaji ,wasindikaji na wadau katika mnyororo wa thamani ya ili kuendeleza sekta hiyo kwa mbinu bora endelevu za kiuchumi na kimazingira.
Kaimu Mkurugezi Idara ya Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) , Mkani Waziri amesema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja kushirikiana na TCCS ili kuona namna wanavyoweza kuleta mageuzi katika tasnia ya ufugaji.
Amesema kuwa wamekuwa washiriki wakuu katika tasnia ya ufugaji ili kuhakikisha watanzania wanafuga kwa tija na kuweza kupata kipato na kukuza uchumi wao.
Waziri amefafanua kuwa mpaka sasa wametoa mikopo kwa wafugaji shilling bilioni 38 ambayo imewanufaisha wafugaji 8,688 katika mikoa 21.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoani Pwani, Ngobere Msamau amesema kuwa kupitia maonesho hayo wanatarajia kupata elimu ambayo inakwenda kuongeza tija katika ufugaji wa kisasa na kuondokana na ule wa kienyeji.