Na. WAF – Dar Es Salaam.
Kambi za matibabu ya madaktari bingwa wa Rais Samia katika hospitali za Halmashauri za wilaya zinasaidia kupunguza rufaa kwa wagonjwa kwenda katika hospitali za kanda na taifa na kupelekea kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.
Hilo limebainika Juni 5, 2024 wakati Daktari bingwa wa upasuaji kutoka hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani- Tumbi Dkt. Tito Lyimo katika kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Ubungo jijini Dar Es Salaam baada ya kumfanyia upasuaji kijana Elia Yacobo Chacha aliyepata ajali ya baiskeli na kuumia eneo la puani.
“Kwa ukubwa wa jeraha Lake, ilikua apewe barua kwenda hospitali ya rufaa ya Mwananyamala lakini kwa sababu ya uwepo wa kambi ya matibabu ya madaktari bingwa wa Rais Samia tumeweza kupatia matibabu ya upasuaji hivyo imempunguzia gharama za matibabu na mzunguko” amesema Dkt Lyimo.
Ameongeza kuwa kupitia kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia inawezesha kutoa mafunzo kwa madaktari wenyeji waliopo kwenye vituo kwenye maeneo mbalimbali ya kutoa huduma
“Tumeweza kutoa mafunzo na kubadilishana uwezo kwenye eneo la matibabu ya upasuaji kwa wagonjwa wenye madhara ya ugonjwa wa TB. Mfano jipu la kwenye mapafu, TB ya uti wa mgongo, TB ya Tenzi za shingoni, TB ya mfumo wa chakula” ameeleza Dkt. Lyimo
Aidha amemshukuru Mkuu wa wilaya ya Ubungo Mhe. Hassan Bomboko kwa mapokezi mazuri na ushirikiano anao utoa kwa madaktari bingwa wa Rais Samia.