Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Korea zimesaini Mkataba wa Mkopo nafuu wa Shilingi bilioni 422.16 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni, Zanzibar.
Mkataba wa Mkopo huo umesaimiwa jijini Soeul Juni 05, 2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kwa upande wa Korea umesaimiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mwandamizi na Mjumbe wa Bodi wa Benki ya Exim – Korea, Mr. Hwang Kiyeon.
Mkopo huo ni moja ya mafanikio ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Korea iliyoanza Mei 31, 2024.
Ujenzi wa Hospitali hiyo utahusisha majengo ya Hospitali yenye vitengo vinne vya magonjwa Maalum kama ya kina mama na watoto, Kituo cha Mafumzo, nyumba za makazi kwa wafanyakazi, ununuzi na ufungaji wa vifaa vya matibabu vya teknolojia ya kisasa na usimikaji wa mfumo wa afya wa mawasiliano.
Uwekaji Saini wa mkataba huo umeshudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango – Zanzibar,
Mhe. Dkt. Saada Mkuya ambaye alieleza kuwa ujenzi huo utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa watu wa Zanzibar, utapunguza idadi ya vifo kutokana na kuimarika kwa huduma bora za afya na matumizi ya vifaa vya kisasa na utahamasisha utoaji wa mafunzo bora ya elimu ya afya kutokana na ujenzi wa Kituo cha Mafumzo kitakachokuwa na vifaa vya kisasa vya kujifunzia.