Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amesema ghorofa lililojengwa katika kiwanja namba 487 Mikocheni jijini Dar es salaam litakabidhiwa kwa Bw. Fatael Anderson baada ya uchunguzi wa nyaraka uliofanyika kubaini kuwa limejengwa na Kampuni ya Jued Homes Limited inayomilikiwa na Bw. Paul Meenda Mushi ambaye awali alitajwa kama tapeli namba moja wa viwanja jijini Dar es salaam.
Waziri Silaa ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara katika eneo hilo akiambatana na mmiliki halali wa eneo hilo Bw. Fatael Anderson ambapo amekuta kiwanja hicho kimejengwa Ghorofa na limekuwa likitumika kwa biashara na ofisi mbalimbali.
Amesema Kiwanja hicho kiliandaliwa hati namba 52250 ya miliki ya miaka 33 kuanzia tarehe 01/01/1984. Hata hivyo Fatael Anderson hakuwahi kusaini rasimu ya hati wala kuchukua hati hiyo ambapo tarehe 12 Machi 2004 Mushi alighushi nyaraka zote kwa kutayarisha hati na kisha kufanya uhamisho wa miliki hiyo kutoka jina la Ndg Fatael Anderson kwenda Kampuni ya Jued Homes Limited.
Silaa amesema tarehe 15/02/2010 kampuni ya Jued Homes Limited walitoa tangazo la kuomba kubadilisha matumizi ya kiwanja kutoka Makazi Kwenda Makazi na Biashara. Mabadiliko hayo yaliidhinishwa na Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji tarehe 20/07/2012.
Katika uchunguzi wa nyaraka imebainika kuwa Kampuni ya Jued Homes Limited (inayomilikiwa na Bw. Paul Meenda Mushi) ilighushi nyaraka zote kwa kutayarisha hati kwa jina la mmiliki Ndg Fatael Anderson na kisha kufanya uhamisho wa miliki hiyo.