Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Bwawani Felician Kamkala akiwa pamoja na Afisa uhusiano Huduma kwa wateja Mkoa wa Kinondoni Kaskazini Flaviana Moshi wakati wa zoezi la utoaji elimu na kushughulikia changamoto za wateja katika mtaa huo.
…………….
Na Sophia Kingimali.
Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kaskazini imezindua wiki ya elimu kwa umma kwa ajili ya kusaidia wananchi wenye changamoto mbalimbali zinazotokana na matumizi ya umeme lakini pia kuwapa elimu ya kujihuduma (TANESCO JISOTI)pindi wanapohitaji kutoa taarifa ya changamoto ya umeme kwenye makazi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 4,2024 katika serikali ya mtaa wa bwawani Makumbusho jijini Dar es salaam Afisa uhusiano huduma kwa wateja mkoa wa Kinondoni Kaskazini Flaviana Moshi amesema lengo la kutoa elimu ni kuhakikisha wanatatua changamoto na kuwafikia wateja kwa ukaribu pamoja na kuwashauri namna bora ya kutumia umeme majumbani ili kuepuka madhara yanayotokana na hitirafu.
Aidha Moshi ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuelezea changamoto zao ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa haraka.
“Hii ni fursa kwa wananchi kujitokeza kujifunza na kutoa changamoto zao zinazotokana na umeme ili tuweze kuwasaidia kwani kwa kiasi kikubwa majanga yanapotokea kwenye majumba ya watu lawama nyingi zinaenda kwa shirika uenda kwa sababu ya wananchi kukosa elimu unakuta utandazaji wa waya kwenye nyumba umewekwa kimakosa na kupelekea matatizo mbalimbali ikiwemo matumizi ya umeme mwingi hivyo ni vyema wakatumia wiki kujifunza hapo makumbusho ndio tumeanza lakini hili ni zoezi endelevu katika hii wiki yote”,Amesema.
Akizungumzia kuhusu huduma ya Jisoti amesema kuwa huduma hiyo ni rafiki kwa kila mtanzania kuitumia kwani inamsaidia kupata huduma kwa haraka pindi anapohitaji pindi anapopiga huduma kwa mteja na kukuta mtoa huduma anahudumia mteja mwingine.
“Hii huduma ya Jisoti imekuja kutatua changamoto za mteja kwani huduma ile ile ambayo ungeweza kuipata pindi unapoongea na huduma kwa mteja sasa unaweza kutumia huduma ya Jisoti kwa kutuma neno Hello kwenda whatsapp no 0748550000 na utachati na kuweza kutatuliwa changamoto zenu”,Amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa bwawani Felician Kamkala amelipongeza shirikisho la umeme TANESCO Kinondoni Kaskazini kwa kufika katika mtaa huo na kutatua changamoto za wananchi lakini pia kwa kuwa karibu wakati wote na kushughulikia changamoto kwa haraka pindi zinapotokea changamoto.
Nao,wakazi wa Mtaa wa bwawani wameipongeza shirika hilo kwa kuweza kuwafikia katika mtaa wao na kukili kujifunza namna mpya ya kuweza kuripoti changamoto zao kwa kutumia huduma ya jisoti ambapo awali walikua hawaifahamu.
“Mimi kiukweli kwa upande wangu nilikua siifahamu kabisa hii huduma ya Jisoti nilikua nategemea kupiga huduma kwa mteja ambapo unatumia muda mwingi kumpata mtoa huduma lakini huduma hii ni rahisi na haraka mimi nitoe wito kwa wananchi wenzangu kutumia huduma hii na nitakuwa barozi mzuri wa kuelezea hili ili watu waweze kuituma ili kupata huduma kwa haraka”,Amesema Saidi Juma mkazi wa Makumbusho.