Mobhare Matinyi
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali
Dar es Salaam, Juni 4, 2024: Saa 8:00 Mchana.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivi sasa yuko ziarani nchini Jamhuri ya Korea kuanzia tarehe 31 Mei, 2024, hadi tarehe 6 Juni, 2024.
Ziara hii ya Mhe. Rais imegawanyika katika sehemu mbili ambapo kwanza ameanza na ziara rasmi nchini humo kufuatia mwaliko wa Rais Yoon Suk Yeol wa Jamhuri ya Korea; na pili amekwenda kuhudhuria Mkutano wa Korea na Afrika akiwa miongoni mwa viongozi kadhaa wa nchi za Afrika.
Serikali ina utaratibu wa kutoa taarifa za ziara za Mheshimiwa Rais mara baada ya kurejea nchini kutoka ziarani ambapo Mawaziri husika, watendaji na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu huzungumza na waandishi wa habari na hivyo wananchi kupata undani wa ziara hizo. Jambo hili litafanyika siku chache zijazo baada ya Mhe. Rais kuwasili nchini.
Hata hivyo, imenilazimu kuchukua nafasi hii mahsusi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa jambo moja tu: Mkopo wa dola za Marekani bilioni 2.5 ulitolewa na Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mkataba wake kusainiwa tarehe 2 Juni, 2024, jijini Seoul. Jamhuri ya Korea hujulikana pia kwa jina la Korea Kusini.
Ufafanuzi huu unafuatia habari yenye dosari iliyorushwa hewani jana na tovuti ya Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Sauti ya Amerika (VoA) na kisha kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuibua maswali ambayo kwa hakika yanahitaji ufafanuzi wa Serikali. Aidha, taarifa hizo pia zimeandikwa na mashirika ya habari ya kimataifa na pia kunukuliwa na magazeti kadhaa nchini na Afrika Mashariki zikiwa pia na upotoshaji.
Katika ziara hiyo, Mhe. Rais ameshuhudia utiaji saini wa nyaraka tatu na tamko moja. Kwanza, ni mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani bilioni 2.5 (sawa na shilingi trilioni 6.7) kwa ajili ya miradi ya miundombinu chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi (Economic Development Cooperation Fund – EDCF) wa Korea.
Mkopo huu kama ambavyo imeshaelezwa na viongozi wengine wanaondamana na Mhe. Rais ziarani, Balozi wa Tanzania nchini Korea, Mhe. Togolani Mavura, na Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, ni wa masharti nafuu ambao utatumia miaka mitano kutolewa lakini utaanza kulipwa baada ya miaka 25, yaani kwenye mwaka wa 26 na kwamba utatumia miaka 40 kulipwa – tofauti na ilivyoelezwa na vyombo vingine vya habari.
Mkopo huu utakuwa na riba ya asilimia 0.01 kwa muda wote wa malipo. Mkopo huu ni kuanzia mwaka 2024 hadi 2028 na ni mwendelezo wa mikopo mingine ya aina hii kutoka Korea kuja Tanzania. Tanzania haijaweka rehani kitu chochote au mali yoyote kama inavyopotoshwa na baadhi ya vyombo vya habari na wanaojadili katika majukwaa mbalimbali ya mitandaoni na yasiyokuwa ya mitandaoni. Mkopo huu si wa masharti ya kuweka rehani kitu chochote.
Tanzania imeshapata mikopo ya masharti nafuu ya aina hii kutoka EDCF ya Korea mara mbili na hii ni mara ya tatu. Mara ya kwanza ilikuwa dola za Marekani milioni 733 (kwa kipindi cha mwaka 2014-2020); na mara ya pili ilikuwa dola bilioni 1 (2021-2025) uliosaniwa Agosti 2021. Huu wa sasa ni wa tatu na unafanya jumla iwe dola bilioni 2.5 kwa kujumuisha na fedha za mwaka 2024 na 2025 wa ule mkopo wa pili.
Tanzania ni moja ya nchini 59 zilizoko barani Afrika, Asia na Ulaya ambazo zinafaidika na mkopo wa aina hii kutoka EDCF.
Mbali na mkataba huo, Mhe. Rais pia alishuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano (MoU) mbili ambapo ya kwanza ni ya ushirikiano katika sekta za uchumi wa bluu ambapo kutakuwa na utafiti, mafunzo na miradi ya uvuvi; na ya pili kwenye madini ya kimkakati ambapo kutakuwa na utafutaji na utafiti, uchimbaji na uongezaji wa thamani kabla ya kuuza bidhaa zake nje, mfano betri za magari.
Aidha, Mhe. Rais alishuhudia kusainiwa kwa Tamko la Pamoja la Uanzishaji wa Majadiliano ya Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (Joint Statement on the Launch of Negotiation on Economic Partnership Agreement – EPA).
Baadhi ya miradi mingine iliyotokana na ushirikiano baina ya Tanzania na Korea na mikopo ya aina hii iliyotajwa hapo juu ni kama ifuatavyo:
Ujenzi wa Hospitali ya Mloganzila;
Uboreshaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili;
Daraja la Tanzanite jijini Dar es Salaam;
Daraja Jakaya Kikwete mto Malagalasi;
Uunganishaji wa mkoa wa Kigoma kwenye gridi ya taifa ya umeme;
Mradi wa maji safi na taka mkoani Iringa;
Awamu ya kwanza ya mradi wa vitambulisho vya taifa vya NIDA;
Bandari ya uvuvi Bagamoyo;
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar;
Hospitali ya Binguni Zanzibar;
Chuo cha Tehama jijini Dodoma;
Mradi wa umwagiliaji Zanzibar.