Kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Miundombonu Ofisi ya Mkuu ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Gilbert Simiya akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed mradi wa ujenzi wa barabara mjini Mbinga ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 99.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Daniel mjini Mbinga ambayo imekaguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed.Mradi huu unasimamiwa na TARURA.
Mradi wa ujenzi wa barabara mjini Mbambabay ambapo serikali imetoa shilingi milioni 500 kutekeleza mradi huu wa barabara yenye urefu wa kilometa 0.8 uliofikia asilimia 99.
…….
Na Albano Midelo,Mbambabay
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeboresha barabara kwa kiwango cha lami katika Wilaya za Mbinga na Nyasa hivyo kuleta unadhifu na mvuto katika miji hiyo.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Mhandisi Silvester Chinengo wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa barabara wilayani Mbinga,Mhandisi Chinengo amesema TARURA ilitengewa kiasi cha shilingi milioni 500 kujenga barabara ya lami nyepesi yenye urefu wa kilometa 0.75,
Amesema ujenzi wa barabara hiyo ulianza Septemba 14,2023 na ulitarajiwa kukamilika Mei 28,2024 ambapo hadi sasa utekelezaji wa mradi huo ni Zaidi ya asilimia 95.
“Mradi huu ni utekelezaji wa mpango wa kujenga barabara za Daniel na Mjimwema wilayani Mbinga,zenye jumla ya kilometa 3.6 mwaka 2022/2023,awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa barabara ya Mjimwema kilometa 1.2 na barabara ya Daniel yenye urefu wa kilometa 2.2 kwa gharama ya shilingi bilioni moja’’,alisema Mhandisi Chinengo.
Hata hivyo amesema awamu ya pili ya ujenzi imehusisha ujenzi wa kilometa 0.9 kwa gharama ya shilingi milioni 500 ,mradi ambao umetekelezwa katika mwaka 2023/2024.
Amesema TARURA inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa kilometa 0.5 zilizosalia kwa gharama ya shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Thomas Kitusi akizungumzia utekelezaji ujenzi wa barabara kiwango cha lami katika Mji wa Mbambabay amesema wilaya hiyo inatekeleza mradi mmoja wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 0.8.
Amesema mradi huo umetengewa shilingi milioni 500 katika bajeti ya mwaka 2023/2024 ambapo hadi sasa mradi umefikia asilimia 99 na kwamba kazi zilizosalia amezitaja kuwa ni kufunga taa tano za kumulika barabarani na kazi ya kuchimba mashimo ya kuweka nguzo.
Ametaja manufaa ya mradi huo kuwa ni kuongeza mtandao wa barabara za lami kutoka kilometa 4.68 zilizokuwepo katika mwaka 2022/2023 hadi kufikia kilometa 5.48,kupunguza gharama za matengenezo na kuleta unadhifu na madhari ya mji.
Akizungumza baada ya kukagua miradi ya barabara hizo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameipongeza TARURA kwa usimamizi wa miradi hiyo ambapo ametoa rai kuhakikisha barabara hizo zinatunzwa ili zitumike kwa muda mrefu.
Ameshauri TARURA kuweka sheria ndogo ndogo zitakazowabana wale wote ambao watafanya uharibifu ili waweze kurejesha uharibufu huo hasa kwa taa za barabarani ambazo zimekuwa zinaharibika mara kwa mara.
TARURA Mkoa wa Ruvuma una mtandao wa barabara zenye jumla ya kilometa 7146.21 zilizosajiriwa.