Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Festo Dugange (Mb) amesema serikali imeendelea kulipa madai ya watumishi wastaafu ambapo itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kulipa kwa awamu madai mbalimbali ya wastaafu kote nchini.
Dkt.Dugange amesema hayo Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha Maswali na Majibu wakati akijibu swali Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini aliyeuliza Je, Serikali itawalipa lini Walimu Wastaafu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa malipo ya Arrears na fedha za kusafirisha mizigo?
“serikali imeendelea kulipa madai ya watumishi wastaafu ambapo hadi kufikia mwezi Mei, 2024 jumla ya shilingi milioni 29.8 kati ya shilingi milioni 31.1 zililipwa ikiwa ni gharama ya kusafirisha mizigo ya walimu 53 kati ya walimu 55 waliokuwa wamestaafu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.”
Amesema hadi kufikia mwezi Mei, 2024 serikali imelipa shilingi milioni 125.3 kati ya shilingi milioni 129.1 ikiwa ni madai ya malimbikizi ya mishahara ya walimu 22 kati ya 25 waliostaafu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
Amesema pia ni haki ya Watumishi Wastaafu kulipwa mafao yao na Salary Arrears na fedha za kusafirisha mizigo kwa wakati na niwajibu wa serikali kuhakikisha wastaafu hawa wanalipwa.