Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amefungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Viungo wa Mikoa na kuwataka kuandaa takwimu zenye uhalisia na taarifa wanazoziandaa kwa wakati.
Dkt. Fatma Mganga ameyasema hayo leo tarehe 4 juni, 2024 katika ukumbi wa VETA Manispaa ya Singida mkoani Singida wakati akifungua mafunzo ya kupitia mpango kazi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 ili kuandaa mpango kazi wa mwaka 2024.
Dkt. Mganga amesema baadhi ya takwimu zinazoandaliwa na Maafisa hao hazina uhalisia na hali hiyo hujitokeza katika miradi ambayo haitegemewi kuwa na idadi kubwa kuzidi maelfu mfano idadi ya madaraja yaliyojengwa na barabara za lami zinazojengwa.
“takwimu zote zinazoingizwa kwenye mipango kazi na taarifa za utekelezaji wa ilani ni muhimu zikahakikiwa kupitia vikao na Wakuu wa Idara husika kuridhia takwimu hizo ili kuwa na uhalisia” alisema Dkt. Mganga.
Aidha, amewaasa Maafisa hao kuhakikisha hakuna utofauti wa malengo yaliyopangwa na taarifa za utekelezaji wa ilani ya CCM lakini pia kuacha kuchelewesha mipango kazi na taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ili kuendana na kalenda ya uwasilishaji wa taarifa katika vikao vya Chama cha Mapinduzi.
Awali akitoa neno la utangulizi kabla ya mgeni rasmi Bw. Johnson Nyingi Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema mafunzo hayo yanahudhuriwa na Maafisa Viungo wa mikoa 26 na baadhi ya Halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam ili kuweza kutatua changamoto ya uandaaji wa taarifa ya Ilani ya CCM kwani kazi nyingi zinafanyika serikalini lakini hazitolewi taarifa.
Naye Bw. Omar Ilyas Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu alisema jukumu la Maafisa hao sio kufuatilia taarifa za utekelezaji bali ni uratibu na ufuatiliaji wa Ilani ya uchaguzi lakini pia uratibu wa shughuli nyingine za Serikali.