Na WAF – Dar Es Salaam
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Mohammed Mang’una amesema uwepo wa kampeni ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia katika Mkoa huo utasaida kuchangia kupunguza Vifo vya Mama na Mtoto.
Dkt. Mang’una amesema hayo Juni 3, 2024 wakati akiwakaribisha jopo la Madaktari bingwa 30 wa Rais Samia kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Albert Chalamila na kusema kuwa Mkoa wa Dar Es Salam una jumla ya zaidi ya wananchi milioni sita na kupelekea idadi ya wagonjwa kuwa wengi hivyo amewataka madaktari bingwa hao kutarajia kuona wagonjwa wengi zaidi kuliko mikoa mingine waliyotoka.
“Pamoja na kwamba mtatuachia ujuzi basi nanyi mtajifunza kutoka kwa Madaktari wa Dar Es Salam, tunaishukuru sana Wizara inayoongozwa na Mhe. Ummy Mwalimu kwa kuweka utaratibu huu wenye lengo la kuwafikishia huduma watanzania pamoja na kubadilisha uwezo na ujuzi baina ya madaktari hawa”. Amesema Dkt. Mang’una.
Aidha, amesema Mkoa wa Dar Es Salam umejipanga kwa kutoa ushirikiano wowote utakao hitajika ili kuhakikisha zoezi la kuwahudumia wananchi linatekelezeka.
Kwa upande wake mwakilishi wa Wizara ya Afya, afisa programu kutoka kitengo cha Huduma za Afya ya Mama na Mtoto Bi. Notgera Ngaponda amewashukuru madaktari bingwa kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kufikisha huduma za matibabu za kibingwa karibu na wananchi na kuongeza kuwa zoezi la madaktari bingwa wa Rais Samia imekuwa na tija kwa watanzania kwa sababu wamekuwa wakijitokeza kwa wingi na bado watanzani wamekuwa na uhitaji mkubwa wa huduma hizi katika maeneo yao.
“Kambi hizi zimekuwa na manufaa makubwa kwa watanzania, toka tuanze kampeni hii tumeweza kuwafikia watu 36,404 tumeona uhitaji wa wananchi ambao walikua wakisumbuliwa na magonjwa mbalimbali kwa muda mrefu ila kupitia madaktari bingwa wa Rais Samia wameweza kupata faraja”.