Na Sixmund Begashe – Bungeni Dodoma
Kijiji cha Makumbusho kimetajwa kuwa na utajiri mkubwa wa urithi wa asili na Utamaduni, ambao unaweza ukawa kichocheo kikubwa zaidi cha utalii wa ndani hasa kwa wakazi wa mijini.
Hayo yamebainishwa Bungeni Jijini Dodoma na Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Janet Elias Mahawanga alipokuwa akichangia kwenye Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka 2024/2025.
Mhe. Mahawanga licha ya kusisitiza uwekezaji zaidi kwenye utalii wa ndani amesema kuwa, Vijana wengi wanaozaliwa mijini wanakosa urithi wa utamaduni wa makabila yao, hivyo wananchi waitumie Makumbusho hiyo kupeleka watoto wao kujifunza na kuwarithisha utamaduni wao.
Aidha Mhe. Mahawanga ameongeza kuwa utajiri huo unapaswa uundiwe program za kila mwezi ili kuvutia watalii wengi zaidi hususani wa ndani.
Naye Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Tabora Mh. Hawa Subira Mwaifunga, ameshauri uwekezaji zaidi kwenye Utalii wa Malikale hususani Mkoa wa Tabora, ili kuvutia Watalii zaidi.