Na Fauzia Mussa, Maelezo.
Afisa Mazingira wa Baraza la Mji Kati Is-haq Kombo Abdallah ameitaka Jamii kudumisha usafi ili kuweka mazingira ya Mji kuwa safi.
Ameyasema hayo huko Unguja Ukuu wakati wa zoezi la usafi wa mazingira, lililowashirikisha wanajamii, viongozi wa afya na Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).
Amesema hali hiyo, itapelekea kuwa kivutio cha wangeni wanoingia nchini na kulipatia Baraza hilo kipato.
Aidha amewataka wananchi kuzidi kushirikiana na baraza hilo katika kulinda Afya ya jamiii kutokana na maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira ikiwemo Malaria na Matumbo ya kuhara na kutapika.
Amefahamisha kuwa jukumu la kufanya usafi linamgusa kila mtu hivyo kitendo cha wanafunzi hao kuamua kuungana na Baraza hilo kufanya usafi ni kizuri na cha kupigiwa mfano na kuigwa.
Ame Suleiman Abdallah ni afisa wa afya na Mwanafunzi kutoka ZU amewaomba Wanafunzi wenzake na jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana na maafisa wa afya katika Baraza hilo ili kuilinda na kuiepusha jamii kutokana na maradhi nyemelezi yanayoweza kujitokeza.
Baraza la Mji Kati, limeweka utaratibu wa kufanya zoezi la usafi kila mwezi ifikapo tarehe 20 katika maeneo tofauti ambapo kwa mwezi uliopita (Mei) zoezi hilo lilifanyika katika Shehia ya Unguja Ukuu Wilaya ya Kati, Mkoa wa kusini Unguja