BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Alexander Mnyeti ameigiza Bodi ya Maziwa kuangalia changamoto za sekta ya maziwa zikiwemo zinazokwaza jamii kunywa maziwa hasa ya kipato cha chini na kuzifanyia kazi.
Ameagiz aleo wakati akifunga maadhimisho ya Wiki ya Maziwa yaliyofanyika Kitaifa jijini Mwanza akisema unywaji wa maziwa kwa Watanzania sasa ni anasa na watoto kutokunywa maziwa wanapata udumamvu sababu bei ya bidhaa hiyo kuwa juu.
“Watanzania kunywa maziwa inaoneakana anasa, kopo dogo la maziwa linauzwa sh.700 haiwezekeni kumpa mtoto akanunue maziwa,zipo familia duni kiasi hicho ni mlo wa siku.Tumewaachia wenye uwezo wanywe pekee yao na kuwakosesha fursa hiyo wasio na uwezo,”amesema Mnyeti.
Amesema TDB ifanyie kazi changamoto hizo Watanzania wanywe maziwa, vinginevyo yatabaki ya kupigia picha sababu ya gharama kubwa huku akiwashauri wasindikaji wa maziwa kutumia vifungashio vya karatasi vinavyotokana na miti kuepuka kutumia mifuko ya nylon (plasitiki).
Naibu Waziri huyo amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amerahisisha ufugaji bora kwa kugawa mbegu za madume bora ya ng’ombe wa kisasa wenye tija, hivyo wafugaji wachangamkie fursa hiyo.
“Rais Dk. Samia pia ameruhusu benki zitoe mikopo kwa wafugaji, changamkieni mikopo hiyo kama wavuvi walivyokopeshwa vizimba.Msilalamike kopeni fedha zipo,hatutaki ng’ombe wa kuzalisha lita tano za maziwa kwa siku na hatutaki mpeleke mifugo yeni kwenye mashamba ya wananchi, kopeni mfuge kisasa,”amesema.
Msajili wa Bodi ya Maziwa,Profesa George Msalya amesema kwa miaka ya karibuni wametumia sh.bilioni 23 kuagiza maziwa nje sababu ya mchango mdogo wa tasnia ya maziwa,watazigeuza changamoto kuwa fursa za kukuza na kuongeza mchango katika uchumi wa nchi.
“Elimu waliyopata wazalishaji na wasindikaji wa maziwa wakaitumie kuongeza mchango katika tasnia kwa kuzalisha maziwa ya unga tuondoe gharama za kuagiza maziwa nje,”amesema.
Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Zacharia Masanyiwa amesema wadau watumie maarifa, elimu na ujuzi waliopata kwa uchumi na maendeleo ya tasnia ya maziwa na kuimarisha uchumi wa kaya nchini.