Kutoka kituo cha TARI Ukiriguru (Mwanza)
Wakulima wa zao la pamba katika Mikoa ya Tabora na Katavi wameendelea kutoa shukrani kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) na Serikali ya Brazil kupitia Mradi wa Cotton Victoria kwa teknolojia ya upandaji mpya zao la pamba ambayo ni sm 60 kutoka mstari hadi mstari na sm 30 kutoka shimo hadi shimo ndani ya mstari kwa mimea miwili kwa kila shimo. Teknolojia hii imesaidia kuongeza tija ya zao la pamba na kipato.
Hayo yamesemwa na wakulima walipotembelewa na watafiti kutoka TARI Ukiriguru mwishoni mwa wiki hii katika ziara iliyolenga kufahamu namna wakulima wanazingatia kanuni za kitaalam za uzalishaji wa pamba.
“Licha ya mabadiliko ya bei ya pamba, bado nimekuwa nikinufaika na zao la pamba tangu nianze kutumia nafasi mpya ya upandaji (sm60Xsm30) kwani nimekuwa nikivuna wastani wa kilo 1500 kwa ekari moja tofauti na wastani wa kilo 300 kwa ekari moja hapo awali. Kwa bei hii ya Tsh.1150 kwa kilo ya pamba inaniwezesha kupata zaidi ya shilingi milioni moja kwa mavuno ya kilo 1500 kwa ekari moja tofauti na kipato cha chini ya laki tano ambayo ningepata kwa kuvuna kilo 300 pekee kwa ekari hapo awali” amesema Bi. Judith Ndolele mkulima wa zao la pamba katika Kijiji cha Itegamatwi, kata ya Ussoke,wilaya ya Urambo mkoani Tabora.
Naye ndugu Ramadhani Nyembe ambaye mkulima mwezeshaji wa zao la pamba mkoani Katavi, amesema “Nimenufaika sana na kilimo cha pamba tangu nianze kutumia nafasi mpya za upandaji ambopo tija ya pamba imeongezeka ukilinganisha na hapo mwanzo nilipokuwa nikipanda kiholela na kupata wastani wa kilo 300-500. Sasa ninauhakika wa kuvuna wastani wa kilo 2200 za pamba kwa ekari.
Ndugu Nyembe pamoja na kunufaika na teknolojia hii ya upandaji wa pamba pia amekuwa balozi mzuri sana kwa kuwahamasisha wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo cha pamba na upandaji mpya. Mapema mwaka 2022 alipewa nafasi na chuo cha maendeleo FDC- Msaginya kilichopo mkoani Katavi kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu kilimo bora cha zao la pamba. Walianzisha shamba darasa la pamba na kutoa nafasi kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Kwa sasa shamba hilo lipo tayari katika hatua ya uvunaji.
Kwa upande wake Dkt. Paul Saidia (Mratibu wa Zao la Pamba Kitaifa na Mkurugenzi wa Kituo- TARI Ukiriguru) amewapongeza wakulima kwa kuendelea kuzingatia kanuni bora za kilimo cha pamba ikiwemo matumizi ya teknolojia mpya ya upandaji wa pamba kwa nafasi ya sm60 x sm30 na kuwaomba kuendelea kuhamasisha wakulima wengine wa zao la pamba. Pia amewakumbusha kupanda kwa nafasi sahihi na kuzingatia kanuni zote za kilimo bora cha zao la pamba pamoja na kukatia ambapo mkulima akipata angalau vitumba 10 kwa mche bado atapata mavuno mengi.
Dkt.Abdullah Mkiga ambaye ni mtafiti wa visumbufu hasa wadudu wa zao la pamba na Kaimu Mratibu wa Uhaulishaji wa Teknolojia na Masharikiano-TARI Ukiriguru aliwakumbusha wakulima kuhusu kutambua wadudu na magonjwa yanayoshambulia zao la pamba na udhibiti. Dkt. Mkiga alisisitiza matumizi ya mbinu husishi za kudhibiti wadudu (IPM) na magonjwa (IDM) kwani zinaongeza ufanisi kwenye udhibiti wa visumbufu hivyo pia ni rafiki kwa mazingira.