KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,akizungumza katika moja ya mikutano yake ya kikazi aliyofanya hivi karibu Unguja.
………….
NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amewasihi wananchi kuwa na tahadhari dhidi ya vyama vya upinzani vinavyoendeleza siasa za choko choko,fitna na uchochezi huku wakikosa sifa ya kupigania maendeleo na kukosa ujasiri wa kutetea maslahi ya umma.
Amesema njia pekee ya kuweka nchi katika hali za Udiwani,Ubunge, Uwakilishi na Urais ili viendelee kuwa wasindikizaji na wapiga porojo katika vijiwe na maskani zao.
Wito huo aliutoa wakati akitoa akichambua masuala mbali mbali ya kisiasa nchini, alieleza kuwa wapo baadhi ya viongozi wa kisiasa wameku mstari wa mbele kutoa kauli za kuingiza nchi katika machafuko ili waweze kuonekana ni majasiri mbele ya wafuasi wao na kusahau kuwa Zanzibar inaongozwa na utawala wa kisheria.
Mbeto,alisema wananchi hawapaswi kuviunga mkono vyama vya upinzani kwakuwa havina sera wala ajenda ya kupigania maendeleo pia hawana uchungu na si watetezi wa rasilimali za Taifa huku akiwataka ACT-Wazalendo kuacha siasa za kuwachonganisha wananchi dhidi ya Serikali yao.
Alisema Chama cha ACT-Wazalendo wamekuwa wakimchafua na kumdhihaki Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia mitandao yao ya kijamii huku wakimtaka atimize matakwa yao ya maridhiano ya kisiasa hali inayoonyesha kuwa viongozi hao hawana chembe ya utu,busara na nidhamu za uongozi.
“Hao jamaa kwa sasa wamechanganyikiwa kwani hawana tena cha kwenda kuwambia wafuasi wao 2025, mambo yote tayari Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kashamaliza utekelezaji wake.
Kwa sasa wanachofanya ni kuzunguka kila kona kutukana na kutoa kauli zisizofaa kwa serikali na viongozi wake yaani wanatoboa jahazi ambalo nao ni wasafiri.”, alisema Mbeto.
Akitoa ufafanuzi juu ya zabuni mbali mbali zinazotangazwa na Serikali kuwa zote zinafuata taratibu zote za kisheria na makampuni yanayoshinda zabuni hizo ndio yanayopewa.
Alisema kitendo cha ACT-Wazalendo kudai kuwa kampuni zinazoshinda zinakuwa na mkono wa Viongozi wa Serikali ni upotoshaji unayotakiwa kupuuzwa vikali kwani madhara yake ni makubwa.
Mbeto, akizungumzia juu ya kauli za ubaguzi wa ukanda na ukabila zinazotolewa wazi na baadhi ya Viongozi wa ACT-Wazalendo kupitia mikutano yao inayoendelea hivi sasa na kusisitiza kuwa siasa za aina hiyo zimepitwa na wakati toka mwaka 1964.
“Kiongozi wa kisiasa unasema hadharani eti watu fulani warudi kwao wawaachie Zanzibar yenu je nyie mnazijua vizuri asili zenu na sisi tuanze kuchimbua mlikotoka?, wenzetu mnatoka katika mstari badala ya kufanya siasa za mleta kauli za mipasho, sisi tutawajibu kwa vitendo kwani tuna kazi ya kujenga nchi.
Aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kuonya juu ya dhambi za ubaguzi leo tunaanza kubaguana kwa wenyewe kwa wenyewe ni hatari kubwa.”alihoji Mbeto.
Alieleza kuwa kauli za wapinzani haziwezi kuzuia kadi ya Serikali katika utoaji wa huduma bora za wananchi.
Alibainisha kuwa CCM inaamini katika maridhiano ya kisiasa lakini sio kwa shinikizo la kauli za kibabe,uchochezi na udalali wa kisiasa na kwamba siasa za aina hiyo hazina dhamira njema ya kuivusha salama Zanzibar.
Katibu huyo wa NEC Mbeto, alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaendeleza siasa za uvumilivu,ustaarabu huku kikinadi sera zake kwa kueleza kwa kina mafanikio na mikakati endelevu ya kuwatumikia wananchi.
Katika maelezo yake Katibu huyo, aliwasihi wanachama,viongozi na watendaji wa CCM kufanya kazi zao kwa ufanisi huku wakiongeza ubunifu katika ufutiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ili iendelee kutoa majawabu chanya ya utatuzi wa changamoto za wananchi.