…………….
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM),Mkoa wa Mwanza kimepongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa utekelezaji wa ilani kwa mafanikio makubwa mkoani humu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu jana,amesema miradi ya maendeleo yenye zaidi ya sh.bilioni 200 imetekelezwa kwa weledi na kupongeza mradi wa Maji Kagunguli-Bukindo kuokoa sh. milioni 326 kati ya sh.bilioni 2.5 za mradi.
“Tunaipongeza serikali,wizara,wabunge na halmashauri,kwa kuisemea na kuisimamia bajeti ya maendeleo ya mkoa wetu,miradi tuliyokagua iko vizuri,hivyo maelekezo tuliyoyatoa wakati wa ukaguzi yazingatiwe ikamilike kwa wakati ”amesema na kuongeza;
“Meneja wa RUWASA Ukerewe,Mhandisi Zubeda Said amefanya kazi nzuri na kuokoa sh.milioni 326 zilizopeleka maji kwa wananchi na taasisi za umma,anastahili pongezi sana.”
Smart amesema uchumi mkubwa wa Mwanza unategemea zao la pamba ambalo uzalishaji wake unashuka kila uchao,hivyo serikali ione namna ya kusimamia na kuboresha kilimo cha zao hilo pia uvuvi usimamiwe vyema kwa kudhibiti uvuvi haramu samaki waongezeke watu wafanye biashara.
“Mkuu wa Mkoa ukiendelea hivi NCU (Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza) itafanya kazi vizuri chini yako.Pia, mwaka huu ni wa uchaguzi wa serikali za mitaa,tuisemee miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali,” aliagiza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda,akiwasilisha utekelezaji wa ilani ya CCM 2020-2025,amesema miradi ya maendeleo ya wananchi ya sh. bilioni 212.7 imetekelezwa mkoani humu ndani ya miaka mitatu.
Amesema miradi hiyo ni ya sekta ya elimu,maji,afya,michezo na miundombinu ya barabara ikiwemo vyombo vya usafiri wa majini.