Mwenyekiti wa Taasisi ya Majlis Al-Maarif Islamiyya Sheikh Tahir Khatib Tahir akimkabidhi Fedha Taslim Bi Zaina Seif mwenye mtoto mwenye ulemavu kwaajili ya kuanzisha biashara, itakayomsaidia kukidhi mahitaji ya mtoto huyo, huko Welezo Wilaya ya Magaharibi A.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Majlis Al-Maarif Islamiyya Sheikh Tahir Khatib Tahir akimkabidhi Fedha Taslim Bi Wanu makame kipenda kwaajili ya kuanzisha Biashara itakayomsaidia kukidhi mahitaji yake na mtoto,huko Mtopepo Wilaya ya Magaharibi A.
……….
Na Fauzia Mussa, Maelezo.
Taasisi ya Majlis Al-Maarif Islamiyya imesema itaendelea kusaidia makundi maalum ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuliyanyua kundi hilo kiuchumi.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Sheikh Tahir Khatib Tahir ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akikabidhi fedha Taslim kwa Wanawake wajane ,wenye Watoto yatima pamoja na akina mama wa Watoto wenye ulemavu Mjini na Vijijini.
Amesema lengo la kutoa msaada huo ni kuwawezesha kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara ndogondogo ili wawaze kujipatia kipato cha kujikimu kimaisha.
Hata hivyo Sheikh Tahir ametoa wito kwa wafadhili na watu wenye uwezo kujitokeza kuiunga mkono Taasisi hiyo ili kufikia malengo waliojipangia.
Sambamba na hayo ameeleza kuwa wanakusudia kuwaunganisha Watoto yatima wanaolelewa katika kituo hicho katika Mfuko wa huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) ili kuwarahishia kupata matibabu.
Katibu wa Taasisi ya Majlis Al-Maarif Islamiyya Jamila Omar Khamis amesema kwa mwaka 2024 wanakusudia kuzifikia zaidi ya Kaya 200 za makundi maalum ili kuweza kunufaika na msaada huo.
Amefahamisha kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu na kueleza kuwa Taasisi itafanya ufuatiliaji wa matumizi sahihi ya Fedha hiyo ili kuona malengo yaliokusudiwa yanafikiwa.
Hata hivyo Katibu Jamila wameahidi kuongeza mitaji kwa kaya zitakazofanya vizuri zaidi ili kuongeza motisha kwa kaya hizo.
Baadhi ya wanufaika wa msaada huo akiwemo Zaina Seif mama wa mtoto mwenye ulemavu, mkaazi wa Welezo, Mtumwa Saleh mkaazi wa Cheju mwenye watoto wawili wenye ulemavu na Zuhura Makame Mjane mwenye Watoto watatu mkaazi wa Tazari wameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwapa mitaji na kuahidi kuitumia kama ilivyokusudiwa.
“Fedha hizi zitatusaidia kukuza mitaji yetu na wale wenzetu waliokuwa hawana kabisa wataanzisha biashara ndogo ndogo,Tunashkuru sana Alhamdulillah.”Walishukuru akinamama hao.
Hata hivyo wamesema mahitaji ya Watoto hao ni makubwa na kuziomba Taasisi nyengine kuwasaidia kwa hali na mali.
Jumla ya sh. milioni mbili zimetumika kwa ajili ya kusaidia Kaya 20 za Wanawake wajane,Wenye Watoto Mayatima na wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ikwemo Welezo, Mtopepo, Dunga, Uroa,Fukuchani na Kidoti ambapo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Taasisi hiyo wakati walipokutana na Wazazi hao katika kipindi cha sikukuu ya Iddil-fitri.