Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro kanali Wilson Sakulo leo tarehe 1 Juni, 2024 amewaaga wananchi 596 ambao walikuwa wakazi wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro na baadaye kufanya maamuzi ya kuhama ndani ya Hifadhi hiyo na Kwenda Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
Akiwaaga wananchi hao, Kanali Sakulo amesisitiza kuwa zoezi la kujiandikisha na kuhama wananchi wa Ngorongoro ni la hiari na serikali itahakikisha kuwa kila mwananchi anayejiandikisha atahamishwa kwa wakati na atapata haki zake zote anazostahili kwa mujibu wa sheria.
“Tunajua kwamba hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la upotoshwaji unaozunguka kwenye baadhi ya vyombo vya Habari kubusu zoezi hili, naomba mzipuuze habari hizo kwa kuwa nia ya serikali ni njema na inalenga kuboresha maisha yenu na mnapewa hiari ya kuchagua wenyewe mnakotaka kuhamia bila kushinikizwa”. Alisema Kanali Sakulo
Kwa upande wake kaimu kamishina wa uhifadhi NCAA Victoria Shayo alisema kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea na zoezi la utoaji wa elimu, uhamasishaji na uwandikishaji wa wananchi hao ambao kwa sasa mwitikio wa uwandikishaji unaendelea kuongezeka na wananchi wengi zaidi wamefikiwa.
Bi. Gladness Ngaluma ambaye ni moja kati ya wananchi walioagwa leo amebainisha kuwa yeye na familia yake wamefanya maamuzi ya kuhamia Msomera kwani waliona kuwa huko watakuwa na uhuru zaidi wa kujiendeleza kwa kufanya shughuli za kiuchumi tofauti ni kuwa ndani ya hifadhi.
“Mimi na familia tumefanya maamuzi ya kuhama Kwenda Msomera kwani huku Hifadhini tunakosa uhuru wa kufanya maendeleo kama kujenga nyumba za kisasa, kilimo, kumiliki vyombo vya moto, uwepo wa wanyama wakali unaoathiri watoto kwenda shule hali inayopelekea tuishi kwenye maisha duni”. alisema Gladness
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo, Meneja wa mradi Afisa wa uhifadhi Mkuu Flora Asey alisema kwamba kufikia leo jumla ya kaya 1,472 zenye watu 8,960 na mifugo 38,098 zimekwisha hama ndani ya Hifadhi kuelekea Msomera na wengine kwenye maeneo waliyochaguwa wenyewe.
Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelee kushirikiana na taasisi zote za kisekta zinazohusika na utekelezaji wa mradi wa kuhamisha wananchi ili kuhakikisha kuwa zoezi linafanyika kwa uwadilifu na wanachi wanapatiwa haki zao wanazostahili kama ilivyoelekezwa na Serikali.