Na Ashrack Miraji Same
ZAIDI ya wakazi elfu nne hamsini na mbili (4052) pamoja na taasisi tano za vijiji vya Msindo na Mbakweni wilayani Same mkoani Kilimanjaro wapo mbioni kuondokana na adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama baada ya Serikali kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.05 kwaajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa.
Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Build Tech Enginnering Company Limited ambapo anatakiwa kuanza utekelezaji wake June 14 mwaka huu na kukamilisha ndani ya siku 365 yaani mwaka mmoja kwa kufanya kazi ya kuchimba mitaro na kulaza bomba umbali wa kilometa 21.3 na kukarabati dakio la maji.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amemtaka mkandarasi kuhakikisha kunakuwa na uwazi wakati wa utekelezaji wa mradi kabla ya kuanza na lazima ashirikiane na viongozi wa Serikali wa vijiji husika ili wananchi waufahamu mradi wao vizuri lakini pia mradi utekelezwe kwa mujibu wa mkataba unavyomtaka.
“Nimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi ambazo amekuwa akizifanya kupitia Wizara ya maji kuhakikisha kero za wakazi wa Same zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati lakini pia nimpongeze Jumaa Aweso Waziri wa maji kwa kutafsiri vyema maono ya Rais wetu ya kumtua mama ndoo kichwani”.Alisema Kasilda.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Same, Amos Kusakula amemsisitiza mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha mradi kwa wakati na kutekeleza kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mkataba ili wananchi waweze kunufaika na fedha zilizotolewa na Serikali.
Naye Diwani wa Kata ya Msindo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Same, Yusto Mapande amewasisi wananchi kuwa pindi mradi utakapo kamilika wanapaswa kujiunga katika jumuiya za watumiaji maji ili waweze kuchangia huduma hiyo kiasi kidogo cha fedha kusaidia kuboresha miundombinu pamoja na uendeshaji wake.