Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoros amekutana na Viongozi wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Comoros (Tanzania Diaspora in Comoros – TADICO) tarehe 30 Mei, 2024 katika Makazi yake, Voidjuu.
Wakati wa mkutano huo, Viongozi wa TADICO walitambulisha Jumuiya yao na kuelezea mikakati wanayoendelea nayo katika kuhudumia wanachama waliojiandikisha na Watanzania wengine wanaoishi au kumtembelea nchini Comoros. Walijukisha kuwa miongoni mwa hatua muhimu ikiyofanyika ni kuwapatia Vitambulisho wanachama 303 Kati ya 374.
Aidha, Viongozi hao walimpongeza Mheshimiwa Balozi Yakubu kwa kuteuliwa kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoros na kuahidi kumpatia ushirikiano ili kumuwezesha kutekeleza majukumu yake kama ilivyo kuwa kwa watangulizi wake. Walimfahamisha kuwa Comoros ni kituo muhimu.
Naye Mheshimiwa Balozi Saidi Othman Yakubu aliwashukuru Viongozi hao kwa kukutana naye ili kubadilishana fikra katika masuala yanyohusu Jumuiya yao pamoja na shughuli zao nchini Comoros.
Aliahidi kutenga muda maalum ili kukutana nao katika makundi yao ili kupata picha zaidi kuhusu harakati zao.
Aidha, aliwajulisha Viongozi wa TADICO kuwa Diaspora ina wajibu wa kuitangaza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoros kwa kutenda yaliyo mema na kuendeleza sifa njema za Nchi yao ikiwemo kuhamasisha umoja na mshikamano katika maeneo wanayoishi, kushirikiana na kutangaza fursa zinazopatikana Tanzania.
Vile vile, aliwafahamisha kuwa, kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kutekeleza mipango kabambe kuhakikisha wanapata fursa ya kuchangia maendeleo nyumbani.