Mwendesha Boda boda kutoka kijiji cha Kilimalondo wilaya ya Nachingwea Frank Manfred na abiria wake aliyefahamika kwa jina la Charles John wakikokota Pikipiki wakati wakivuka katika mto Lumesule unaotenganisha wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na Nachingwea mkoa wa Lindi.
Muonekano wa Barabara inayotoka kijiji cha Pacha ya Mindu kwenda kijiji cha Ngapa mpakani mwa mikoa ya Ruvuma na Lindi ambayo inahitaji kujengwa kwa lami ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
…………………..
Na Mwandishi Wetu
Tunduru
WAKAZI wa kijiji cha Ngapa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na wakazi wa kijiji cha Kilimalondo wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi,wameiomba Serikali kupitia wizara ya ujenzi kujenga daraja katika Mto Lumesule ili kuwanusuru wasiendelee kupoteza miasha kwa kusombwa na maji na kurahisisha mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili.
Charles John mkazi wa kijiji cha Kilimalondo wilayani Nachingwea alisema,daraja katika mto huo lina umuhimu mkubwa kwani litawawezesha kuwa na mawasiliano ya uhakika majira yote ya mwaka na kufanya shughuli za usafi na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Frank Manfred alisema,kwa muda mrefu mto Lumesule umekuwa hatari kwa maisha yao hasa watoto wadogo na wanawake wanasombwa na maji pindi wanapotaka kwenda wilaya jirani ya Tunduru kufuata huduma mbalimbali za kijamii kama vile matibabu na chakula.
Alisema,pindi maji yanapojaa katika mto huo ambao ni mpaka wa mikoa ya Ruvuma na Lindi,wanalazimika kutumia gharama kubwa kati ya Sh.5,000 kwa mtu na Sh.15,000 kuvusha pikipiki pindi wanapotaka kuvuka kwenda upande mwingine.
Aidha alisema,kukosekana kwa daraja katika eneo hilo kunawarudisha nyuma kiuchumi kwa sababu wanashindwa kwenda upande wa Tunduru ambako ni karibu zaidi kwa ajili ya kufuata baadhi ya huduma za kijamii na kufanya shughuli za uchumi ikiwemo uchimbaji wa madini ya vito yanayopatikana kwa wingi upande wa wilaya ya Tunduru.
Hamis Mfaume(Papaa)alisema hali hiyo sio kwa kwa sababu ya mvua tu,bali ni tatizo la miaka mingi na hata kusababisha kijiji chao kuwa kama kisiwa kutokana na mto huo kujaa maji mengi wakati wote wa mwaka.
Mkazi wa kijiji cha Mnazi Mmoja kata ya Ngapa wilaya ya Nachingwea Sofia Bule alisema,licha ya kukosekana kwa daraja litakalounganisha kata yao na wilaya ya Nachingwea,lakini pia barabara inayotoka Pacha ya Mindu hadi kijiji cha Ngapa ni mbovu.
Ameiomba serikali,kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha barabara na kujenga kwa kiwango cha lami ili waweze kuwa na mawasiliano ya uhakika kuliko hivi sasa ambapo kila inapofika wakati wa masika barabara hiyo haipitiki kirahisi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ngapa Yasin Likenge ameishauri serikali, kuacha kusubiri hadi watu waendelee kupoteza maisha ndipo ijenge daraja katika eneo hilo, badala yake ione umuhimu wa kujenga daraja haraka ili kunusuru maisha ya wananchi wake.
Alisema,serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kujenga daraja katika eneo hilo,lakini bado haijatekeleza huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa daraja ambalo litasaidia sana kuharakisha maendeleo ya kijiji na kata ya Ngapa kwa ujumla.
Mhandisi kutoka ofisi ya meneja wa TANROADS)Mkoa wa Ruvuma Irene Kapinga alisema,Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS)imeanza maandalizi ya kujenga daraja katika mto Lumesule ili kuunganisha mawasiliano ya wananchi wa wilaya mbili za Nachingwea na Tunduru mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa Kapinga,kazi zilizofanyika hadi sasa ni kufanya usanifu na upembuvu ambapo kazi ya ujenzi wa daraja hilo itafanywa kwa ushirikiano kati ya TANROADS mkoa wa Ruvuma na Lindi.
Kapinga,amewaomba wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati huu ambako serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan iko mbioni kuanza ujenzi wa daraja hilo.