MAMLAKA ya mapato Nchini (TRA) imewataka wafanyabiashara Mkoani Geita kuhakikisha wanalipa kodi zao kwa awamu ya pili ya malipo ya kodi ya mapato kabla ya Juni 30, 2024 ambapo zoezi hilo litasitishwa rasmi.
Wito huo umetolewa na Ofisa Elimu kwa mlipakodi na mawasiliano, Makilo Seuta wakati akizungumza na waandishi mapema leo 31 Mei 2024, kwenye Viwanja vya maonesho ya Fahari ya Geita ambayo yanaendelea kwenye viwanja vya EPZA Mjini Geita.
Amesema kupitia maonyesho hayo wameendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa wanachi na wafanyabiashara kujua wajibu wao wa msingi wa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka na usumbufu.
“Tupo kwenye maonyesho ya fahari ya Geita kwaajili ya kutoa elimu na kuwaambia wafanyabiashara umuhimu wa kutoa kodi tunatambua baadhi wanajua suala la ulipaji wa kodi lakini kazi yetu sisi ni kuwapa elimu pamoja na kuwakumbusha wajibu wao mkubwa wa kuchangia maendeleo ya Nchi kupitia Kodi ambayo wanaitoa kwa hiari.
“Sisi kama mamlaka ya mapato hatupendi kuwasukuma wafanyabiashara na wananchi juu ya ulipaji kodi tunapenda wafanye kwa hiyari” Amesema Makilo.
Aidha Makilo amesema elimu ambazo wameendelea kuzitoa ni pamoja na elimu kuhusu masuala ya biashara kwa mtu anayetaka kujifunza namna ya kulipa kodi kupitia biashara anayoifanya na kiasi sahihi cha kodi.
“Lakini pia tunatoa namba za malipo ya kodi na pia tunatoa elimu ya biashara ya magendo ambayo baadhi ya watu wamekuwa wakifanya biashara hizo ambapo ni kinyume cha sheria ya nchi kwani kufanya magendo ni sawa na kuiibia Nchi.” Amesema Makilo.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingarame amefika kwa ajili ya kutembelea mabanda na kujionea shughuli mbalimbali za wajasiriamali, amesema maonesho ya Fahari ya Geita yamekuwa ya kipekee kutokana na uwepo wa washiriki wengi kutoka ndani ya nchi na Nje ya nchi.