Na Albano Midelo,Mbambabay
SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 81 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa bandari ya Mbambabay ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mhandisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Fabian Paul wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bandari ya Mbambabay kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ambaye amefanya ukaguzi wa eneo la ujenzi wa mradi huo mjini Mbambabay.
Mhandisi Paul amesema TPA Desemba 2023 iliingia mkataba wa miezi 24 na Kampuni ya M/S Xiamen Ongoing Constructio Group ya nchini China kwa ajili kuanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa bandari ya Mbambabay.
Amesema mradi wa ujenzi wa bandari hiyo mpya unatarajia kukamilika Januari 26,2026 ambapo amezitaja kazi zinazofanyika kuwa ni usanifu,ujenzi wa gati lenye uwezo wa kuegesha meli mbili zenye uzito wa tani 5,000 na ujenzi wa jengo la utawala.
Mhandisi Paul ameyataja majengo mengine kuwa ni ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari,ujenzi wa jengo la abiria,ghala na karakana,ujenzi wa barabara za ndani na mzunguko,kuchimba kwa ajili ya kuongeza kina cha maji eneo la kupaki na maingilio ya meli,kuweka mifumo ya umeme,maji,ulinzi,ujenzi wa uzio na kujenga eneo la sakafu ngumu lenye ukubwa wa mita za mraba 20,000 kwa ajili ya kuhudumia shehena.
Hata hivyo amesema utekelezaji wa mradi huo hadi sasa umefikia asilimia 35 katika ukusanyaji wa vifaa na mitambo ya ujenzi,ujenzi wa ofisi kwa ajili ya mradi umefikia asilimia 75,kazi ya usanifu wa kina imefikia asilimia 25 na kazi ya kutoa mawe eneo la ujenzi imefikia asilimia 20.
“TPA inatoa shukurani za dhati kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha taslimu shilingi bilioni 81 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huu mkubwa katika ziwa Nyasa’’,alisema.
Ameutaja mradi huo ukikamilika,makao makuu ya bandari za Ziwa Nyasa yanatarajia kuhama kutoka Kyela mkoani Mbeya na kuhamia Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Akizungumza baada ya kukagua eneo la mradi wa bandari ya Mbambabay,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanalii Ahmed Abbas Ahmed amesema kukamilika kwa bandari hiyo kutaongeza ukuaji wa uchumi wa Taifa na Mkoa na kwamba mradi huo pia utatengeneza ajira kwa vijana.
Amesisitiza kuwa bandari ya Mbambabay itaiunganisha Tanzania na mataifa mengine ya Msumbiji na Malawi hivyo kuimarisha Zaidi mahusiano na mataifa hayo na kukuza uchumi.
Mkuu wa Mkoa ameiagiza TPA kulipa haraka fidia za barabara,makaburi na fidia zingine ili wananchi waweze kupisha utekelezaji wa mradi na kwamba wahakikishe wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika hatua za utekelezaji wa mradi huo ili waone mradi ni wao.
“Zile kazi ambazo si za kitaalam sana tuwape wananchi wetu wa maeneo haya,lakini hata zile kazi za kitaalam ambazo watu wetu wanaweza kufanya wapewe kipaumbe wao kwanza kabla ya kutoka nje ya Mkoa’’,alisisitiza.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameipongeza Kampuni inayotekeleza mradi huo kwa kuwa na vifaa muhimu ambapo ameagiza kuongeza vifaa Zaidi na nguvu kazi ili kutekeleza mradi huo ndani ya mkataba.
Amesisitiza kuwa atafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo kwa sababu mradi huo unachukua sura ya kimataifa na kiuchumi ambapo mradi unaweza kusaidia kukuza uchumi na kuongeza mapato.