Na. Zillipa Joseph Katavi
Mwanafunzi mmoja wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya St. Mary’s iliyopo katika manispaa ya Mpanda mkoani Katavi; aliyejulikana kwa jina la Luis Emmanuel (17) amefariki baada kudaiwa kunywa kemikali inayodhaniwa kuwa ni Ethanol.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi S.A.C.P Kaster Ngonyani amesema tukio lilitokea mei 25; mwaka huu majira ya saa tano asubuhi wakati wanafunzi hao wakifanya usafi katika chumba cha maabara cha shule hiyo.
Kamanda Ngonyani amewataja wanafunzi wengine waliokunywa kemikali hiyo kuwa ni Evangelist Deodatus ambaye anaendelea na matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Katavi na Anastazia Zakayo ambaye alitibiwa na anaendelea na masomo.
Akizungumzia tukio hilo baba mzazi wa marehemu Mashaka Nkana amesema alipata simu kutoka shuleni kuwa mwanae anaumwa na alifika kwa ajili ya kumpeleka hospitali.
Bwana Nkana anasema alimpeleka mtoto wake kutibiwa katika zahanati ya Monica na baadaye hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Katavi.
Siku ya Jumapili madaktari waliniita wakasema hali ya mwanangu si nzuri na apelekwe rufaa hospitali ya Bugando. Nilikubali na tulimpeleka Bugando ambako ndiko mauti ilipomkuta siku ya jumatatu” alisema Nkana.
Mkuu wa wilaya ya Mpanda bi. Jamila Yusuf amesema wanaendelea kuchunguza tukio hilo na kutoa rai kwa walimu kuongeza usimamizi pindi wanafunzi wanapoingia maabara.