Na Fauzia Mussa, Maelezo.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amewataka Waandishi wa habari chipukizi kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo kushindania  Tuzo ili  kujitangaza katika jamii.

Ameyasema hayo katika hafla ya kutunuku tuzo kwa washiriki wa shindano la kumtambua mwaandishi wa Habari Chipukizi na mbunifu kwa jamii ya SUZA 2024  huko idara ya mawasiliano na mafunzo ya Habari (SUZA) Kilimani wilaya ya Mjini.

Amesema endapo tuzo kama hizo zitaandaliwa mara kwa mara, zitasaidia kuwajengea uwezo waandishi wa habari chipukizi wa kuweza kufanya kazi zao kwa bidii.

Amefahamisha kuwa fani ya uandishi wa Habari ni taaluma inayohitaji ufahamu wa masuala mbalimbali hivyo amewakumbusha Vijana hao kuendelea kujifunza zaidi ili kuimarisha na kukuza vipaji vyao.

Sambamba na hayo amewataka waandishi hao kujikita zaidi kujifunza lugha za kigeni ikiwemo lugha ya kichina ili kuweza kufanya mawasiliano  na wageni wanaoingia nchini jambo ambalo litawasaidia  kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hata hivyo Kitwana amewataka washindi wa tuzo hiyo kutobweteka na badala yake waongeze baidii ili  kukuza na kuendeleza vipaji vyao  hadi kufikia kuwa waandishi mahiri wa habari.

Kwa upande wake Mkuu wa idara ya mawasiliano na mafunzo ya Habari SUZA Dkt. Khamis Juma Abdalla amesema lengo la tuzo hiyo ni kutambua mchango wa wanafunzi na wahitimu wa kada ya habari na mawasisliano wa chuo hicho katika  kuihabarisha jamii juu ya  masuala mbalimbali yanayohusiana SUZA.

Aidha amewapongeza vijana hao kwa kushiriki katika tuzo hiyo  na kusema  kuwa tuzo hiyo itakuwa endelevu ili kuongeza ujuzi na kukuza vipaji vya vijana hao.

Mwenyekiti wa kamati ya majaji katika tuzo hiyo Dkt. Saleh Yussuf Mnemo ameeleza kuwa jumla ya vijana 40 wenye umri kati ya miaka 18 -35 waliwasilisha kazi zao, kati ya hizo  17  ziliingia kwenye mchujo zikiwemo  10 za washiriki Wanawake.

Aidha Dk. Mnemo ameiomba SUZA kushirikisha Waandishi wa Habari walio nje ya chuo hicho ili kuimarisha shindano hilo katika tuzo zijazo.

Nao baadhi ya Waandishi waliotunukiwa tuzo katika shindano hilo wameishukuru SUZA kwa kuanzisha mashindano hayo kwani imekuwa chachu ya kuamsha ari katika utendaji wa kazi zao za kila siku.

Aidha wamezishauri taasisi nyengine kuiga mfano wa Chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA) katika kuandaa tuzo kama hizo ili kusaidia kukuza vipaji vya waandishi chipukizi.

Jumla ya Vipengele 10 vilishindaniwa katika tuzo hiyo ambapo katika kipengele cha upigaji picha (photojournalism) mshindi ni Fauzia Mussa Abdalla kutoka Idara ya habari Maelezo Zanzibar, uwaandaji wa vipeperushi(FLAYERS)  ni Khamis Juma Omar, mtangazaji bora ni Rehema Shaibu Kombo, Makala ni Ali Mussa Kinasa ,makala za mtandaoni ni  Bakari  Massoud, lugha ya kichina ni Ali Abas na  kwa upande wa kipengele cha mshereheshaji hakukua na mshiriki.