Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Juni 16, 2026
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani, Zainab Vullu, amewasihi wazazi na walezi kuimarisha malezi ya watoto kwa kuwajenga katika misingi ya maadili, hususan watoto wa kiume ambao kwa sasa wanakabiliwa na hatari zinazotokana na mazingira hatarishi na mmomonyoko wa maadili.
Amesema taifa haliwezi kuwa na maendeleo endapo watoto wa kike na wa kiume hawatalelewa katika maadili mema, hivyo akasisitiza umuhimu wa wazazi kuwa karibu na watoto na kufuatilia mienendo ya ndani na nje.
Vullu alitoa rai hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya UWT katika Manispaa ya Kibaha, ambapo alikagua mradi wa vyoo salama vinne katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha pamoja na chumba maalumu cha uzazi na upasuaji katika Kituo cha Afya Kongowe, sambamba na kuzungumza na wanachama wa jumuiya hiyo.
“Wazazi wengi wamekuwa bize na shughuli za kutafuta kipato kiasi cha kukosa muda wa kukaa na watoto wao, ni muhimu kuzungumza nao, kuwafuatilia na kuwajenga katika maadili mema ili kuwaepusha na athari za matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na utandawazi,” alieleza Vullu.
Alieleza kwamba, vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vimeongezeka katika jamii, huku watoto wakikumbwa na matukio ya ubakaji, ulawiti na aina nyingine za ukatili, hali inayohitaji ushirikiano wa jamii nzima katika kuwalinda watoto.
Vilevile aliwataka wanawake kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya kukuza mitaji ya biashara zao badala ya kukimbilia mikopo ya mitaani ambayo mara nyingi huibua migogoro na kudhoofisha ustawi wa familia.
Kwa upande wake, Katibu wa UWT Mkoa wa Pwani, Aziza Omari, alifafanua lengo la ziara hiyo ni kuwashukuru wanachama wa UWT na Watanzania kwa kuipa ushindi CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, sambamba na kukagua miradi ya maendeleo na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama.
Naye Katibu wa UWT Kibaha Mjini, Cecilia Ndallu, alisema jumuiya hiyo imefanikiwa kuinua uchumi kwa kujenga mgahawa, ofisi za jumuiya katika kata tano kati ya kata 14 zilizopo wilayani hapo huku Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini, Elina Mgonja, akiwapongeza wanawake kwa kujitokeza kwa wingi katika ziara hiyo.
Mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha, Selina Koka, alisema wanaendelea kushirikiana kuimarisha shughuli za jumuiya hiyo, akibainisha kuwa Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, amechangia vitanda 20 vyenye thamani ya shilingi milioni tano kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia wanafunzi.

