Na John Bukuku
Watumishi saba wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni pamoja na mzabuni mmoja wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Manyoni wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali ya uhujumu uchumi yakiwemo utakatishaji fedha unaodaiwa kuhusisha zaidi ya Sh milioni 501 za Serikali.
Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi Na. 13485/2026 ilifunguliwa Juni 16, 2026 dhidi ya aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, George Mzeru, pamoja na maafisa mahesabu Emilian Mauki, Lutufyo Mwakapala, Edward Kilumbu, Revania Ruheta, Doreen Shirima na Salum Mafita. Mshitakiwa mwingine ni mzabuni wa kampuni ya ML Kimboka General Trading, Michael Mushi.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ambayo ni utakatishaji fedha, kuongoza genge la uhalifu, kuisababishia mamlaka husika hasara, wizi wakiwa watumishi wa umma, ufujaji pamoja na ubadhirifu.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Julai 1, 2024 hadi Mei 29, 2026 na kusababisha hasara kwa Serikali.
Mashtaka hayo yalisomwa mahakamani na Wakili wa Serikali, Godfrey Songolo, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, Ailisile Mwankejela.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi wala kutoa dhamana.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 30, 2026 kwa ajili ya kutajwa huku uchunguzi ukiendelea.
