Na Fauzia Mussa, Maelezo.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amewataka Waandishi wa habari chipukizi kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo kushindania Tuzo ili kujitangaza katika jamii.
Ameyasema hayo katika hafla ya kutunuku tuzo kwa washiriki wa shindano la kumtambua mwaandishi wa Habari Chipukizi na mbunifu kwa jamii ya SUZA 2024 huko idara ya mawasiliano na mafunzo ya Habari (SUZA) Kilimani wilaya ya Mjini.
Amesema endapo tuzo kama hizo zitaandaliwa mara kwa mara, zitasaidia kuwajengea uwezo waandishi wa habari chipukizi wa kuweza kufanya kazi zao kwa bidii.
Amefahamisha kuwa fani ya uandishi wa Habari ni taaluma inayohitaji ufahamu wa masuala mbalimbali hivyo amewakumbusha Vijana hao kuendelea kujifunza zaidi ili kuimarisha na kukuza vipaji vyao.
Sambamba na hayo amewataka waandishi hao kujikita zaidi kujifunza lugha za kigeni ikiwemo lugha ya kichina ili kuweza kufanya mawasiliano na wageni wanaoingia nchini jambo ambalo litawasaidia kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hata hivyo Kitwana amewataka washindi wa tuzo hiyo kutobweteka na badala yake waongeze baidii ili kukuza na kuendeleza vipaji vyao hadi kufikia kuwa waandishi mahiri wa habari.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya mawasiliano na mafunzo ya Habari SUZA Dkt. Khamis Juma Abdalla amesema lengo la tuzo hiyo ni kutambua mchango wa wanafunzi na wahitimu wa kada ya habari na mawasisliano wa chuo hicho katika kuihabarisha jamii juu ya masuala mbalimbali yanayohusiana SUZA.
Aidha amewapongeza vijana hao kwa kushiriki katika tuzo hiyo na kusema kuwa tuzo hiyo itakuwa endelevu ili kuongeza ujuzi na kukuza vipaji vya vijana hao.
Mwenyekiti wa kamati ya majaji katika tuzo hiyo Dkt. Saleh Yussuf Mnemo ameeleza kuwa jumla ya vijana 40 wenye umri kati ya miaka 18 -35 waliwasilisha kazi zao, kati ya hizo 17 ziliingia kwenye mchujo zikiwemo 10 za washiriki Wanawake.
Aidha Dk. Mnemo ameiomba SUZA kushirikisha Waandishi wa Habari walio nje ya chuo hicho ili kuimarisha shindano hilo katika tuzo zijazo.
Nao baadhi ya Waandishi waliotunukiwa tuzo katika shindano hilo wameishukuru SUZA kwa kuanzisha mashindano hayo kwani imekuwa chachu ya kuamsha ari katika utendaji wa kazi zao za kila siku.
Aidha wamezishauri taasisi nyengine kuiga mfano wa Chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA) katika kuandaa tuzo kama hizo ili kusaidia kukuza vipaji vya waandishi chipukizi.
Jumla ya Vipengele 10 vilishindaniwa katika tuzo hiyo ambapo katika kipengele cha upigaji picha (photojournalism) mshindi ni Fauzia Mussa Abdalla kutoka Idara ya habari Maelezo Zanzibar, uwaandaji wa vipeperushi(FLAYERS) ni Khamis Juma Omar, mtangazaji bora ni Rehema Shaibu Kombo, Makala ni Ali Mussa Kinasa ,makala za mtandaoni ni Bakari Massoud, lugha ya kichina ni Ali Abas na kwa upande wa kipengele cha mshereheshaji hakukua na mshiriki.