Wananchi wa Wilaya ya Liwale wameonesha furaha yao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na huduma bora wanazozipata kutoka kwa madaktari bingwa kupitia program ya Mama Samia mentorship.
Wakizungumza na vyombo vya habari jana jumatano katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale ambapo huduma hizo zinatolewa, wananchi hao wamesema kuwa wanamshukuru Rais kwa kuwapelekea Madaktari bingwa ambao wamekuwa msaada wa matatizo ya afya kwa wananchi wengi wa wilaya hiyo.
Ndg. Nassor Mtimbo mkazi wa Liwale B, amewaeleza Waandishi wa Habari kuwa anamshukuru Mhe. Rais kwa kuwasambaza Madaktari bingwa katika maeneo ambayo wananchi wengi hawana uwezo wa kusafiri maeneo ya mbali kufuata huduma za kibingwa.
Aidha, Mzee Chande Said ambaye alifika hospitalini hapo kupata huduma ameeleza kuwa huduma hii ya Madaktari bingwa kutoka Hospitali tofauti tofauti hapa nchini ni jambo ambalo halijawahi fanyika katika kipindi chote cha umri wake.
Mzee Chande ameongeza kwa kumshukuru Mhe. Rais kwa kuwa ameokoa maisha ya wananchi wengi wa Wilaya ya Liwale na watanzania kupitia program hii ya Madaktari bingwa.
Kwa upande wake, Dkt. Fredrick Mabena ambaye ni daktari bingwa wa mfumo wa mkojo pamoja na uzazi kwa wanaume amesema kuwa ndani ya siku mbili zaidi ya wagonjwa 30 wamejitokeza wakiwa na matatizo ya ngili maji ambapo tayari wagonjwa 12 kati ya hao wameanza kufanyiwa upasuaji.
Dkt. Mabena amewaasa wananchi wenye changamoto za kiafya zinazohitaji huduma ya upasuaji wajitokeze katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale ili wapate matibabu kwa gharama ndogo.