Afisa Haki Miliki kutoka COSOTA akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la MUHAS
Afisa Haki Miliki kutoka COSOTA, Bi Mwanaisha Sendekwa akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kutoa elimu kwa wabunifu kutoka MUHAS wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu
Bi Mwanaisha Sendekwa akitoa elimu kuhusu Haki Miliki kwa wabunifu kutoka MUHAS.
……………
Mapema leo wabunifu kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili (MUHAS) wamepatiwa mafunzo kuhusu umuhimu wa kulinda maslahi ya bunifu zao, kutunza rejista za usajili wa kazi za kibunifu ili kupata uthibitisho wa umiliki ( copy right clearence) na kulinda kazi zao.
Akizungumza na wabunifu kutoka MUHAS, Afisa Haki Miliki kutoka COSOTA, Bi. Mwanaisha Sendekwa alisema uthibitisho wa umiliki ni haki ya kipekee ambayo inampatia mtunzi au mbunifu kipato kutokana na ubunifu wake na pia ni bidhaa ambayo huweza kuuzwa kwa mtu mwingine na kubadilisha umiliki.
” Ni muhimu kila mbunifu anapobuni ubunifu wa kazi yake anakuwa na haki miliki na haki ya kiuchumi na haki za kimaadili ambazo zinasaidia usuluhishi wa migogoro ya uvunjifu wa haki miliki pale unapotokea” Alisema Bi. Mwanaisha.
Mkutano huu uliandaliwa na Mratibu wa Ubunifu kutoka MUHAS, Dkt. Nelson Masota kwa lengo la kuwakutanisha wabunifu kutoka MUHAS na mtaalamu wa COSOTA ili wapate elimu husika kuhusiana na masuala ya haki miliki.
Na pia aliahidi kuwaalika wataalamu hao kutoka COSOTA kuja MUHAS ili watoe elimu hiyo kwa kina zaidi kwa wabunifu wa MUHAS.
Mkutano huu ulifanyika leo kwenye maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya shule ya sekondari Popatlal , jijini Tanga.