JIBU: ANC ni miongoni mwa rafiki zetu wa kweli. Duniani hapa kuna vyama vingi vya siasa. Nikiri hapa, ANC ni moja ya vyama vilivyo kwenye moyo wangu, kiitikadi.
Miongoni mwa rafiki zangu wa utotoni wakati nikikua miaka ile ya 80 pale Kinondoni Biafra, ni watoto wa ANC. Kwamba wazazi wao walikuwa wapiganaji wa ANC na waliishi mtaa wa nyuma yetu, Mtaa wa Kanazi ‘ D’. Tuliishi barabara ya Kawawa, zamani Morocco Road.
Nyumba ile ya ANC ingalipo( Pichani yenye geti.)
Serikali yetu iliwapa hifadhi watu wa ANC kwenye nyumba ya ghorofa. Tulicheza wote mtaani, na baadae kwenye timu moja pale viwanja vya Biafra.
Oh! Ni watoto wale ambao sasa ni wa umri wangu na wenye kuipambania ANC isitoke madarakani.
Ningetamani kuwa kwenye mitaa ya Soweto, Mafikeng, Mamelodi na kwengineko Afrika Kusini, niwepo huko kushiriki nao mapambano;
“ Amandla.. Ngawethu!”
Nilijiua kwa mara ya kwanza maana ya salamu hiyo enzi zile za utoto wetu. Sisi na watoto wenzetu wa ANC.
‘ Amandla’ ina maana ya ‘ Power’- Nguvu kwa Kiswahili. ‘ Ngawethu’ ina maana ‘ to Us’. ‘ Kwetu’- kwa Kiswahili.
Nawakumbuka pia kaka zetu wale vijana wa ANC walioishi pale Kanazi Street, Biafra Kinondoni. Wengine walikuwa wenye jazba sana.
Kuna waliopelekwa Mazimbu, Morogoro. Ni kwa mafunzo ya kijeshi. Walirudi wakakamavu tayari kupelekwa kwenye uwanja wa mapambano.
Pale Kanazi Street, Biafra walikuja vijana wasomi sana wa ANC. Walikuja kusalimia wenzao wakitokea Mazimbu, Morogoro. Kuna siku sikuamini kumwona anayezungumza pale barazani alikuwa Flaxman Wa Qoopane. Huyu jamaa nilikuwa nasoma sana mashairi yake ya Ukombozi kwenye Daily News na Sunday. Yalikuwa mafupi na yenye ujumbe wenye nguvu.
Ni katika mazingira kama yale nilijisemea, kwamba lazima nisome sana.
Flaxman alikuwa kijana na bado masomoni kule Solomon Mahlangu Freedom College, Mazimbu, Morogoro. Flaxman akaja kuwa mshairi na mtunzi wa vitabu. Akawa bingwa wa fasihi.
Kwangu ANC, ukiacha changamoto kinazokipitia, kinabaki kuwa ni chama chenye mikakati ya Kisayansi sana.
Ndio, kina wapanga mikakati mahiri. Ni wenye kupanga, kuweka malengo na kutengeneza njia za kuyafikia malengo yao.
Nimeifuatilia kwa karibu ANC, Kimsingi, kabla 1994, ANC waligawa harakati zao kwenye maeneo matatu makuu;
Kijeshi ( Military), Kiitikadi ( Ideology)na Kiichumi( Economy/Business)
Hilo la kwanza lilihusisha mafunzo ya kijeshi pia ndani na nje ya Afrika Kusini, mfano wa Dakawa na Mazimbu kule Morogoro.
Tanzania ina mchango mkubwa kwa jeshi letu kutoa mafunzo ya kijeshi kwa makada wa ANC. Aidha, kwa watu wa Intelijensia ya Tanzania kutoa mafunzo kwa makada wa ANC.
Kimsingi, ANC wanakiri wenyewe, kuwa hawajui namba bora ya kuishukuru CCM na watu wa Tanzania.
Umkhoto we Sizwe ( Mkuki wa Taifa)
Ndivyo lilivyojulikana tawi la kijeshi la ANC. Wapiganaji aina ya Chris Hanni, walitajwa sana kwenye harakati hizo.
Kwenye Itikadi ANC walikuwa vizuri sana. Kuna kizazi cha mafisadi wachache walio ndani ya ANC wenye kuharibu taswira njema ya ANC ndani na nje ya Afrika Kusini. Ni hao wenye kuigharimu ANC.
Vinginevyo, ANC kiitikadi ni wenye misimamo. Kwenye siasa za Kimataifa ndio kabisa. Hawapindishi wakiamini jambo, mathalan, chini ya ANC, Afrika Kusini ndio taifa pekee duniani ambalo halikuishia tu kuishutumu Israel kwa yanayofanyika Gaza. Afrika Kusini chini ya ANC imeibuluza Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa.
Kiuchumi, ANC walishajipanga zamani. Hata kabla ya Ukombozi wao kutoka kwa Makaburu. ANC walikuwa na mikakati ya kuwapa mafunzo ya masuala ya uchumi na kuendesha biashara kwa baadhi ya makada wao.
Kwenye kundi hilo kuna makada waliosomea pia Ujasusi wa Kichumi. Ni makada aina ya Cyril Ramaphosa.
Ramaphosa akaja kuwa mfanyabiashara maarufu ( Biashara nyingine hazikuwa zake). Na msomaji usiniulize zilikuwa za nani?
Kimsingi, ANC walikuwa na vitega uchumi vya kimikakati ili kukijengea uwezo chama chao.
Hivyo, walijiandaa Kujitegemea kwa kuwa na vitega uchumi kwenye nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania.
Si wengi wenye kufahamu, kuwa zilipo ofisi za Benki ya Dunia, Dar es Salaam, Mirambo House, ni jengo la ANC.
Wanachofanya ANC ni kuwekeza na kuendesha biashara kwa kuingia ubia na kampuni binafsi.
Si wengi pia wenye kufahamu, kuwa ANC ni Chama cha Siasa tajiri kushinda vyote, sio tu Afrika, bali duniani.
ANC wakiondokana na viongozi wachache wenye kutanguliza maslahi binafsi, bado wana nafasi ya kuijenga Afrika Kusini yenye neema na maisha bora kwa wengi. Ikawa mfano kwa vyama vingine Afrika.
Tuna kila sababu za kuwatakia Heri na matokeo mema ya Uchaguzi rafiki zetu wa kweli, ANC.
Afrika Kusini itakayoongozwa na Serikali iliyoundwa na ANC hatutakuwa na chembe nayo ya mashaka.
“ Amandla … Ngawethu…!”
Maggid Mjengwa.