MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea Mhandisi Chionda Kawawa amesema mradi wa umeme uliozinduliwa na Mwenge wa uhuru mwaka 2024 utachochea shughuli za maendeleo na kukuza uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea Mhandisi Chionda Kawawa alisema kuwa ili kupata maendeleo na uchumi kwa wananchi lazima kuwepo na nishati ya umeme kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Mhandisi Kawawa alisema kuwa kuwepo wa umeme wa kutosha, kutachangia wananchi kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo zitakuza uchumi wa wananchi wa wilaya ya Nachingwea.
Alisema kuwa wananchi wa wilaya ya Nachingwea wanamshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusaidiana kukuza uchumi wa wananchi wa wilaya ya Nachingwea.
Mhandisi Kawawa aliwataka wananchi kuendelea kuitumza miundombinu ya umeme ambayo serikalini imewekeza kwa ajili ya maendeleo na kujipatia kipato na kukuza uchumi wao.