Na WAF – Geneva, Uswisi
Utashi wa Kisiasa na Uongozi imara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto ni moja ya jambo ambalo limechangia Tanzania kupunguza vifo vya wajawazito kutoka vifo 556 hadi 104 katika kila vizazi hai 100,000.
Waziri Ummy amesema hayo leo Mei 28, 2024 kwenye Mkutano uliojadili mikakati ya kupunguza vifo vya wajawazito ambao umeandaliwa na Umoja wa Afrika, Wizara ya Afya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa Afya ya mama na mtoto anbao ni EGPAF na SAVE THE CHILDREN.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan toka akiwa Makamu wa Rais aliasisi Kampeni mahususi ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto sambamba na kuwasainisha mikataba Wakuu wa Mikoa ili kuwajibika katika maeneo yao katika suala hili.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amebainisha mbinu nyingine zilizotumika hadi kufanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito kutoka vifo 556 hadi 104 katika kila vizazi hai 100,000 ni pamoja na kuimarisha ubora wa huduma ikiwemo uwajibikaji katika ngazi zote za utoaji huduma za Afya nchini.
“Hatua nyingine ni kuwepo kwa sharti linalotaka kituo/Hospitali yoyote inayopata kifo cha mjamzito kufanya mapitio ya kila kifo cha mjamzito katika vituo vya umma ndani ya masaa 24 na kuweka mpangokazi ili kisitokee kifo kingine.” Amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema, uwekezaji katika miundombinu ya upasuaji kwa wajawazito, dawa za uzazi salama na uwepo wa mfumo wa Rufaa wa dharua kwa wajawazito M-Mama, ushirikishwaji wa vyama vya kitaaluma vimefanikisha Tanzania kupata mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vya wajawazito.
Kwa upande wake Kamishna wa Huduma za Afya na Maendeleo ya jamii wa Umoja wa Afrika Balozi Minata Samata wakati akifungua Kikao hicho amesema, Umoja wa Afrika utaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kuyafikia malengo ya agenda namba 63 ambayo yanalenga kuwa na kizazi chenye Afya kwa wote hususani wanawake, watoto na vijana.
Vilevile ameeleza kuwa, kupitia Kampeni ya CARMMA itasaidia sana kuyafikia malengo namba 3.1 na 3.2 ya malengo ya Dunia ya maendeleo endelevu.