Na WAF – Geneva, Uswisi
Wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya waipongeza Tanzania kwa kuanzisha mpango jumuishi na shirikishi wa wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii utakaowafikishia wananchi huduma za Kinga, Tiba na Elimu ya Afya mahali walipo bila vikwazo vyovyote.
Wadau hao wameipongeza Tanzania baada ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kuwaeleza umuhimu wa kuwatumia wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) ikiwa ni mkakati wa kuimarisha utoaji wa huduma za Afya ngazi ya msingi na kufikia lengo la Afya kwa wote.
Waziri Ummy amesema hayo Mei 28, 2024 kwenye Mkutano uliofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 77 wa Shirika la Afya Duniani (WHO), unaoendelea Jijini Geneva nchini Uswisi uliowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, Taasisi za Kimataifa pamoja na mashirika yasiyo ya Kiserikali ya ndani na nje ya nchi.
“Wadau hawa pia wameahidi kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa mpango utakaoleta mabadiliko na kuboresha Afya za wananchi ikiwemo kutoa rasilimali watu na fedha kwa kuendelea kuwatumia wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii.” Amesema Waziri Ummy
Katika mkutano huo pia uliambatana na mdahalo wa wataalam wabobezi wa Afya ngazi ya msingi kutoka ndani na nje ya nchi ambao walieleza kwa kina na kwa ushahidi namna mpango huo utakavyoleta mabadiliko na kuboresha Afya za wananchi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema Serikali imejipanga kutekeleza mpango huo katika Mikoa yote 26 na Halmashauri 184 za Tanzania lengo likiwa ni kufikia vijiji vyote 12,318, Mitaa 4,263 na vitongoji 64,384 kwa kuwa na watoa huduma za Afya ngazi ya Jamii wawili wawili na hivyo kuwa na jumla ya wahudumu laki 137,294.
Mkutano huo ambao uhudhuriwa na washiriki zaidi ya 200 wakiwemo Mawaziri wa Afya kutoka nchi za Afrika na mabara mengine, umedhihirisha wazi matarajio na mategemeo ya wadau kuwa mpango huo utakuwa wa mfano katika kuboresha uratibu wa afua mbalimbali za Afya zinazotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Wadau waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Umoja wa Afrika, Shirika la Afya Duniani, UNICEF, Global Fund, Botnar Fondation, Susan Buffet Thompson Foundation (STBF), PEPFAR, CDC, Swiss – TPH na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi.