Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana ili kuwa na mpango madhubuti wa kukabiliana na majanga ya asili au yale yanayosababishwa na binadamu ili kupunguza athari zitokanazo na majanga hayo.
Prof. Janabi ametoa wito huo leo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Tiba ya Magonjwa ya Dharura ambayo hufanyika kila mwaka Mei, 27 sambamba na uzinduzi wa Muongozo wa Hospitali wa jinsi ya kutoa huduma wakati wa majanga (Emergency and Disaster Preparedness Guideline) pamoja na zoezi la kupima utayari wa watoa huduma wa hospitali hiyo katika kukabiliana na majanga pale yanapotokea lililofanyika leo asubuhi.
Prof. Janabi amesema Jiji la Dar es Salaam linakua kwa kasi, kuna majengo marefu ambayo ikitokea changamoto inabidi tuwe na vyombo mahsusi vya kukabiliana na changamoto hiyo kulingana na urefu wa jengo husika.
Naye Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhumbili (MUHAS), Dkt. Doreen Kamori amesema ni muhimu kuchukua tahadhari na kuelimisha jamii juu kutunza mazingira ili kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi kwani maafa yanapotokea huzalisha majeruhi ambao huhitaji huduma za dharura ikiwemo uokozi, matibabu na mara nyingi hutokea nje ya hospitali.
“Ikumbukwe siku ya magonjwa ya dharura ilianzishwa kwa mara ya kwanza Mei 27, 2018 kwa lengo la kujenga utaratibu utakaowawezesha wananchi, watalaam wa afya, wadau wa afya, watunga sera na wanasiasa kutafakari na kujadili uboreshwaji wa tiba ya dharura katika maeneo yao na kuonesha umuhimu wa kuwepo na mfumo imara wa huduma za dharura unaoratibiwa vizuri ili kuokoa maisha au kupunguza athari ya dharura na ajali inapotokea”, amesisitiza Dkt. Kamori.
Amesema karibia watu bilioni 3.6 duniani wanaishi kwenye maeneo hatarishi yanayoweza kukumbwa na mabadiliko ya tabia nchi na inakadiriwa kufikia mwaka 2030 hadi 2050 kutakuwa na ongezeko la vifo 250,000 hadi 300,000 vitokanavyo na athari ya mabadiliko ya tabia nchi. Kauli mbiu ya mwaka huu ni MABADILIKO YA TABIA NCHI, PIA NI DHARURA YA KIAFYA